1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barrow amteua mwanamke kuwa makamu wa rais

24 Januari 2017

Rais wa Gambia, Adama Barrow amemteua Fatoumata Jallow-Tambajang kuwa Makamu wa Rais. Huo ni uteuzi wa kwanza tangu Barrow alipochukua madaraka Januari 19.

https://p.dw.com/p/2WIZb
Gambia nach Präsidentschaftswahl - Wahlsieger Adama Barrow
Picha: Reuters/A. Sotunde

Barrow ambaye bado yuko nchi jirani ya Senagal alikotafuta hifadhi kwa sababu za kiusalama, amesema amemteua mwanamke huyo Fatoumata Jallow-Tambajang kushika wadhifa huo wa juu, kwa sababu ya kushughulikia usawa wa kijinsia.

Fatoumata mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, ni mtu muhimu ambaye aliviunganisha vyama vya upinzani kusimama pamoja katika uchaguzi dhidi ya kiongozi wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh.

Gambia Fatoumatta Tambajang
Fatoumata Jallow-Tambajang (kulia) akiwa na kiongozi wa chama cha UDP, Ousainou Darboe (Kushoto)Picha: picture alliance/abaca/Y. Sama

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Fatoumata aliliambia gazeti la The Guardian kwamba atamfungulia mashtaka ya uhalifu Jammeh. Muda mfupi baada ya tangazo hilo, Jammeh ambaye sasa yuko uhamishoni Equatorial Guinea, alibadili uamuzi wake wa awali wa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Disemba Mosi, na kudai kulikuwepo na udanganyifu, hali iliyochochea mzozo wa kisiasa.

Aidha, Fatoumata ameitaka tume ya taifa ya kudhibiti mali, kuzirejesha mali na ardhi ambayo inadaiwa kuchukuliwa na Jammeh kwa maslahi yake mwenyewe.

Barrow kurejea leo Gambia

Msemaji wa Serikali ya Gambia, Halifa Sallah, amesema serikali yote ya Barrow itatangazwa baadae leo. Jammeh, aliivunja serikali yake, ambapo nusu yao tayari walikuwa wameshajiuzulu, wakati wa mzozo wa kisiasa baada ya kukataa kuondoka madarakani na kukabidhi uongozi kwa Barrow. Akizungumza jana na waandishi wa habari, Sallah alisema Barrow Jammeh anapanga kurejea leo nchini Gambia.

''Rais Barrow anajiandaa kurejea kesho. Tunatarajia kuona mipango zaidi kwa sababu makamu wa rais ataanza kazi. Nina uhakika mtapata taarifa nzuri zaidi kuhusu  kipindi hiki cha mpito kwake na hivi karibuni kipindi hicho kitamalizika na atakuwa nchini na kutakuwa na sherehe katika uwanja wa uhuru kama ilivyopangwa hapo kabla. Na watu wataanza awamu mpya ya Gambia mpya iliyoamuliwa na watu wa Gambia,'' alisema Sallah

Makundi ya kutetea haki za binaadamu yalidai kuwa idara za kiusalama zilikuwa chini ya udhibiti binafsi wa Jammeh na walihusika kwa mauaji yasiyo halali, utesaji pamoja na kuwakamata watu kiholela.

Gambia Machtwechsel - Menschen fahren nach Banjul zurück
Maelfu ya Wagambia waliokimbia nchi wakirejea nyumbaniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema diplomasia ilitumika kuzuia umwagikaji wa damu, kurejeshwa kwa demokrasia na kuepuka maafa ya kibinaadamu nchini Gambia. Msemaji wa umoja huo, Stephane Dujarric amesema kama diplomasia isingefanya kazi vizuri, ingeshuhudiwa hali mbaya zaidi.

Dujarric amewaambia waandishi wa habari kwamba umoja ulioonyeshwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ambao uliungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ulikuwa muhimu kwa Jammeh kukabidhi madaraka kwa Barrow. Afisa wa shirika la kibinaadamu la Umoja wa Mataifa, Toby Lanzer amesema Wagambia 45,000 ambao walikimbilia Senegal na 7,000 waliokimbilia Guinea Bissau, sasa wanarejea nyumbani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP
Mhariri: Daniel Gakuba