1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua pepe za Emmanuel Macron zadukuliwa

Caro Robi
6 Mei 2017

Timu ya kampeini za mgombea urais wa Ufaransa Emmanuel Macron imesema barua pepe zake zimesambazwa mitandaoni baada ya kompyuta zake kudukuliwa kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/2cWAB
Frankreich Wahlkampf Emmanuel Macron
Picha: Getty Images/S. Lefevre

Macron anayeelemea siasa za mrengo wa kati amelaani kudukuliwa kwa barua pepe zake. Haijabanika wazi ni nani amezidukua na kuzisambaza data hizo siku moja kabla ya uchaguzi. Kulingana na uchunguzi wa maoni ya wapiga kura, Macron atashinda kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura dhidi ya Marine Le Pen, mgombea wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Front 

Wanaoendesha kampeini za Macron wamesema kudukuliwa na kusambazwa kwa maelfu ya barua pepe, nyaraka zinazoonesha matumizi ya kifedha ya timu ya kampeini na nyaraka nyingine nyeti ni jaribio la kile wamekitaja kuhujumu demokrasia kama ilivyoshuhudiwa katika kampeini za uchaguzi wa rais nchini Marekani mwaka jana.

Macron apigiwa upatu kumshinda Le Pen

Nyaraka hizo zilisambazwa katika mitandao ya kijamii Ijumaa usiku wakati Macron mwenye umri wa miaka 39 na mpinzani wake Le Pen walipohitimisha rasmi kampeini kuelekea duru hiyo ya pili ya uchaguzi.

 Washirika wa Macron wamesema kuvujishwa kwa barua pepe za timu ya kampeini ni jambo ambalo halikutarajiwa katika kampeini za uchaguzi mkuu Ufaransa. Barua pepe hizo zilisambazwa na mtu au kundi linalojiita EMLEAKS. Inasemekana nyaraka hizo ziliibwa majuma kadhaa yaliyopita baada ya akaunti binafsi za barua pepe za maafisa kadhaa wa chama cha Macron En Marche kudukuliwa.

Bildkombo Wahlkampfplakate Frankreich
Wagombea urais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Marine Le Pen

Umoja wa Ulaya umeweka wazi kwamba unatarajia kuona ushindi wa kinyang'anyiro cha urais nchini Ufansa unakwenda kwa Emannuel Macron kutokana na khofu ya kitisho kinachosababishwa na Le Pen anayeupinga Umoja wa Ulaya.

EU na Obama wamuunga mkono Macron

Maafisa kadhaa waandamizi wa Umoja huo wa Ulaya wakiongozwa na rais wa halmashauri ya Umoja huo Jean Claude Junker wamevunja miiko yao ya kawaida katika chombo hicho ya kutoingilia kati chaguzi za ndani ya mataifa na kuzungumzia wazi kumuunga mkono mwanasiasa huyo wa siasa za wastani ambaye ni mfanyakazi wa zamani wa benki na aliyekuwa waziri wa uchumi wa Ufaransa Le Pen.

Umoja wa Ulaya unamuona Macron kuwa msitari wa mbele kupinga siasa kali za kizalendo na unaamini kwamba Ufaransa chini ya Macron itaendelea kubakia mwanachama wa Umoja huo. Hata Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amemuunga mkono Macron na kusema kwamba mtazamo wa Macron unavutia watu kwa kuwapa matumaini na sio kwa kutumia hofu zao.

Uamuzi wa Obama kumuunga mkono Macron pia unatofautiana na wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alisema Le Pen ni mzuri zaidi katika masuala ya mipaka ya nchi na chaguo bora kwa Ufaransa yenyewe. Katika duru ya kwanza Emmanuel Macron, alijipatia asilimia 24.1 ya kura naye Le Pen mwenye umri wa miaka 48, alijipatia asilimia 21.30 ya kura.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/dpa

Mhariri: Sudi Mnette