Barua ya wazi ya CPJ kwa rais wa Tanzania Magufuli
13 Agosti 2019Barua hiyo ya wazi kwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli imeeleza kwamba ni mwezi uliopita tu wakati wa mkutano wa kutetea uhuru wa vyombo vya habari mjini London, waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania Palamagamba Kabudi amethibitisha kwamba serikali yake inataka "kuwezesha uandishi habari wa kiuchunguzi" na "kuhakikisha kwamba waandishi habari wanalindwa dhidi ya hatua zozote, kushitakiwa ama kukamatwa." Kumruhusu Kabendera kurejea katika kazi yake, na kulichukulia kwa dhati suala la kupotea kwa Gwanda, litakuwa hatua muhimu kuelekea kutimiza ahadi hizi.
Kabendera alichukuliwa kwa nguvu kutoka nyumbani kwake Julai 29, 2019, na kunyimwa uwezekano wa kuwakilishwa na wakili kwa zaidi ya kipindi cha masaa 24. Polisi awali walidai kwamba wanachunguza uraia wa Kabendera. Hata hivyo, siku chache baadaye baada ya kukamatwa kwake waendesha mashitaka walibadilisha njia na kumshitaki kwa uhalifu wa kiuchumi, mashitaka ambayo hawezi kupata dhamana.
Kuhojiwa Kabendera
Alihamishwa katika vituo mbali mbali vya polisi katika wakati wa kuhojiwa. Utaratibu wa kukamatwa kwake na kushikiliwa kunaonesha kulipizwa kisasi ambako kunaelekea kutaka kunyamazisha hatua yake ya uandishi wa kukosoa, ikiwa ni pamoja na migawanyiko ndani ya chama tawala.
Gwanda pia alifanya kazi kama mwandishi wa kujitegemea, katika eneo la mkoa wa pwani. Alipotea Novemba 21, 2017, akiwa pamoja na watu ambao hawajajulikana wanaoaminika kuwa watu wa usalama wa taifa, barua hiyo ya CPJ imeandika.
Katika mahojiano mwezi Julai mwaka huu, waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania Kabudi alidai kuwa Gewanda alikuwa mmoja wa watu wengi ambao, kwa maelezo yake "walipotea na kufariki" katika wilaya ya Rufiji, licha ya kuwa Kabudi baadaye alisema matamshi yake yalichukuliwa vibaya, na hafahamu hatima ya Gwanda. Matamshi yake shirika la CPJ linasema yanaleta ukakasi na kuonesha umuhimu wa haja ya uchunguzi w kile kilichomkuta mwandishi huyo.
Shirika la CPJ pia limesema linakaribisha fursa ya kukutana na wawakilishi wa serikali kujadili wasi wasi huu. DW imejaribu kuwatafuta wasemaji wa serikali kuzungumzia barua hii lakini hatukufanikiwa.