Bashir aionya Sudan Kusini
19 Aprili 2012Akiongea kwa kujiamini huku anacheza na kupunga fimbo yake hewani, Rais el Bashir alisema yeyote atakaye sogeza mkono wake kwa Sudan, basi mkono huo utakatwa. Bashir amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wakaazi katika mji mkuu wa jimbo la Kordofan wa El-Obeid. Bashir amesema hatakubali hata kipande kidogo cha nchi kichukuliwe na Sudan kusini
Bashir aliendelea kubashiri kuwa katika masaa machache majeshi yake yataukomboa mji wa Heglig, na akaongeza kuwa mgogoro kati ya nchi yake na Sudan ya Kusini hautaisha hadi pale utawala wa kusini utakapoanguka ingawa hakusema ni lini hili litatokea. Bashir alisema hadithi hii iliyoanzia heglig, inaweza kuishia Khartoum au Juba.
"Wasudan wenzangu, wakati wa kueleza ukweli umefika, tutafia Juba au Khartoum. Watu wa Sudan, vijana, tuko tayari kwa vita, Mwenyezi Mungu akipenda, tutawashinda wadudu wa SPLA, Mungu akipenda, tutawashinda," alisema rais Bashir.
Juhudi za kusuluhisha zaendelea
Wakati Bashir akiyasema hayo, mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu Sudan na Sudan Kusini, Princeton Lyman, alikuwa anatembelea eneo hilo katika jitihada za kusuluhisha mgogoro huo unaotishia kuzipeleka nchi hizo katika vita vikubwa.
Muda mfupi baada ya rais Bashir kutoa matamshi hayo, Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini alisema majeshi yake yamezuia uvamizi uliyokuwa umepangwa kufanyika katika mji wa Heglig lakini hakukuwa na kauli yoyote kutoka Sudan kuhusu madai hayo. Siku ya Jumatano, nchi hizi zilishtumiana kwa kwa kufanyiana mashambulizi ambapo jeshi la sudan kusini liliripoti vifo vya wanajeshi 22
Marekani yaonyesha wasiwasi
Akizungumzia matamshi ya rais Bashir, msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani Mark Toner, aliwaambia waandishi wa habari kuwa matamshi hayo yanaongeza wasiwasi wa kuzidi kwa uhasama kati ya nchi hizi mbili.
Toner alirejelea wito wa Marekani kwa Sudan ya Kusini kuondoa majeshi yake katika mji wa Heglig, na kwa serikali ya Khartoum kukomesha mashambulizi ya angani.
Taarifa ya Wizara hiyo imesema Lyman, ambaye alifanya mazungmzo na rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir mapema, alitarajia kuzungumzo na maafisa wa serikali ya Sudan jijini Khartoum.
Tatizo ni mafuta
Mataifa yote ya Sudan yanategema mafuta kwa uchumi wake na kutokea kwa vita kunaelezwa kuathiri uchumi wa nchi hizi vibaya. Hali ya kutoaminiana inazidi kuzifarakanisha nchi hizi hasa kuhusu suala la mipaka, na kiasi gani Sudan ya Kusini inapaswa kulipa ili kutumia miundombinu ya Sudan kusafirisha mafuta yake. Mjini Juba, kiasi ya watu 1,000 walikusanyika na kuimba nyimbo za kumkejeli Bashir na walimkosoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwa kauli yake ya kuitaka Sudan Kusin iondoe majeshi yake kutoka Heglig.
Alfred Lado Gore, Waziri wa Mazingira na Afisa mkuu wa chama cha SPLM naye alimkosoa Ban Ki-Moon na kusema kama Sudan Kusini iliweza kushinda vita vya uhuru, pia itashinda Heglig na jimboni Abyei.
Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Sudan, Omer Mohamed aliwaambia waandishi wa habari kuwa Sudan itaendelea kutumia njia za kidiplomasia na kijeshi kurejesha mji wa Heglig.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetishia kuziwekea vikwazo nchi hizi mbili endapo hazitasitisha mapambano. Lakini Sudan imesema vikwazo hivyo yafaa vielekezwe kwa Sudan Kusini inayoilaumu kwa kuingilia uhuru wa mipaka yake.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE\APE
Mhariri: Moahammed Abdul-Rahman