1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bashir hatahudhuria mkutano wa nchi za maziwa makuu Zambia

15 Desemba 2010

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Sudan atamuwakilisha rais Bashir kwenye mkutano huo wa kilele wa nchi za maziwa makuu utaojadili matumizi haramu ya madini

https://p.dw.com/p/QZ16
Rais wa Sudan, Omar Hassan al-BashirPicha: picture-alliance/ dpa

Serikali ya Zambia inasema rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, anayetafutwa kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita, hatahudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za maziwa makuu hii leo mjini Lusaka, unaolenga kudurusu masuala ya mazingira. Hata hivyo kiongozi huyo atamtuma waziri wake wa mambo ya kigeni. Taarifa hiyo imetangazwa na redio ya kitaifa ya Zambia hapo jana.

Zambia ilikuwa imemualika rais Bashir kuhudhuria mkutano huo licha ya waranti uliotolewa mwaka jana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague Uholanzi. Msemaji wa serikali ya Zambia amesema polisi ya nchi hiyo haingemkamata kama angehudhuria kikao hicho. Viongozi wa upinzani nchini Zambia wameukosoa uamuzi wa kumualika rais Bashir, anayetakikana kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki katika kuukandamiza upinzani katika jimbo la Darfur. Mataifa kadhaa ya Afrika na mengine hayajatekeleza waranti huo.