Bastian Schweinsteiger atundika madaluga
29 Julai 2016Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Bastian Schweinsteiger ameamua kuondoa mchango wake katika timu ya taifa. Mchezaji huyo wa kati mwenye umri wa miaka 31 anayesakata kandanda katika timu ya Manchester United ya England , ambaye alishiriki kwa mara yake ya 120 katika jezi ya Die Mannschaft katika mchezo wa nusu fainali wa Euro 2016 ambao Ujerumani ilishindwa kwa mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa , amefichua taarifa hizo katika ukurasa wake wa Twitter jana Ijumaa.
Anastaafu kucheza timu ya taifa wakati majaaliwa yake katika kikosi cha kocha Jose Mourinho wa Manchester United hayafahamiki, ikiripotiwa kwamba ameambiwa ni mmoja kati ya wachezaji tisa watakaopigwa kalamu na mwalimu huyo nyota.
Schweinsteiger bado ana miaka miwili katika mkataba wake na United.
Maumivu ya goti aliyoyapata mwezi Januari mwaka huu yaliongezeka katika mwezi wa Machi , yakimzuwia kucheza katika klabu yake kwa ukamilifu na kufanikiwa kushiriki katika michezo michache tu kabla ya kucheza katika kinyang'anyiro hicho cha kombe la Ulaya , akifunga bao moja dhidi ya Ukraine katika mchezo wa kwanza wa Ujerumani katika kundi lake.
Mchezaji huyo kiungo mkabaji amesema sasa ni wakati muafaka wa kustaafu katika timu ya taifa kabla ya mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu kwa ajili ya michezo ya fainali za kombe la dunia mwaka 2018 dhidi ya Norway hapo Septemba 9, siku nne baada ya mchezo wa kirafiki nyumbani dhidi ya Finland.
"Nimemfahamisha kocha wa taifa Joachim Loew asinifikirie tena katika uteuzi wake wa timu ya taifa hapo baadaye kwa kuwa ningependa kuweka darini madaluga yangu nitumiayo kwa timu ya taifa" Schweinsteiger ameandika katika ukurasa wake wa Twitter.
"Ningependa kuwashukuru mashabiki , timu, chama cha soka nchini Ujerumani na makocha.Katika mara 120 nilizoruhusiwa kucheza katika timu yangu ya taifa nilishuhudia nyakati ambazo haziwezi kuelezeka na za mafanikio makubwa," amesema Schweinsteiger.
Bastian Schweinsteiger ni mmoja kati ya wachezaji wanaoitwa wa kizazi cha dhahabu katika timu ya taifa ya Ujerumani , ambapo kimefanikiwa kuleta taji la kombe la dunia , mwaka 2014 kutoka Brazil.
Ugonjwa wa Zika
Hatari ya ugonjwa wa virusi vya Zika katika michezo ya Olimpiki iko chini na inaweza kushughulikiwa bila matatizo , amesema mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, wiki moja kabla ya tukio hilo kuanza katika mji mkuu wa Brazil Rio de Janeiro.
Karibu watu nusu milioni wanatarajiwa kuhudhuria michezo hiyo, wengi wao kutoka Marekani. Hofu juu ya usalama , virusi vya Zika na mzozo wa kiuchumi vinaweza kuzuwia wasafiri, wakati ni chini ya robo ya tiketi za tukio hilo bado hazijanunuliwa.
Brazil imeathirika pakubwa na kuzuka kwa ugonjwa huo, na wataalamu wengi wa masuala ya afya , washiriki wa mashindano hayo na watazamaji wameeleza hofu yao kwamba michuano hiyo ya Olimpiki inaweza kuwa nyenzo ya kusambaa kwa virusi hivyo duniani.
Yulia Stepanova
Mfichuaji wa kashfa ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu za misuli kwa wanamichezo doping, nchini Urusi Yulia Stepanova , amesema kwamba yeye si msaliti kwa nchi yake. Hatua yake ya kufichua uovu huo uliokuwa ukitendwa kitaifa karibu uigharimu timu nzima ya Urusi kupigwa marufuku kushiriki katika michezo hiyo mjini Rio de Janeiro. Stepanova amesema alikuwa anajaribu kusema ukweli, kwa kuwa ameshuhudia wachezaji wengi wakiharibikiwa katika wakati wao wa uanamichezo.
"Ningependa kuomba radhi kwa kilichotokea hapo zamani. Nilitumia dawa za doping na hivi sasa sisemi hilo kama kisingizio, lakini ni kuelezea kile kilichokuwa kinatokea, unahitaji kuwa ndani ya kile kilichokuwa kinatokea kufahamu hilo."
Kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC imemualika mkimbiaji huyo wa mbio fupi na mume wake kuhudhuria michezo hiyo kama mgeni mwalikwa lakini kamati hiyo imemkatalia kushiriki michezo ya Rio, ikidai kuwa matumizi yake ya dawa hizo hapo zamani yanamfanya kutokubalika kushiriki mashindano hayo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu