1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern bado ni mlima mrefu katika Bundesliga

3 Machi 2014

Katika Bundesliga , Bayern Munich sasa yafanya tu mazowezi na timu za ligi hiyo na si kushindana,yaibugiza Schalke 04 mabao 5-1, Borussia Dortmund yajisogeza katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi.

https://p.dw.com/p/1BIj2
Fußball Bundesliga 23. Spieltag FC Bayern München - FC Schalke 04
Bayern wakishangiria baoPicha: picture-alliance/dpa

Timu zote katika ligi ya Ujerumani zinatafakari vipi zinaweza kuizuwia Bayern Munich msimu huu. Kila timu inayokutana na Bayern inatafakari tu jinsi ya kupunguza madhara, Schalke 04 haikuwa tofauti siku ya Jumamosi jioni wakati ilipoingia katika uwanja wa nyumbani wa Bayern, Allianz Arena na kujikuta ikichambuliwa kama karanga.

Baada ya kipigo cha mabao 6-1 Jumatano iliyopita dhidi ya Real Madrid ya Uhispania katika mpambano wa Champions League, Schalke ilijikuta katika hali ya kupimana uwezo kati ya Bayern na Real na nani anaweza kupachika mabao mengi zaidi dhidi ya timu hiyo.

Fußball Bundesliga 23. Spieltag FC Bayern München - FC Schalke 04
Arjen Robben akipachika bao kwa BayernPicha: Getty Images/AFP

Bayern yavuna ilichopanda

Hali hiyo iliiacha Schalke ikiwa haina msaada. Bayern walikuwa wakifanya watakavyo katika muda wote wa dakika tisini na wachezaji wa Schalke walikuwa wakifukuza kivuli tu. Bayern walionesha mchezo wa hali ya juu na wa kasi kupita uwezo wa wachezaji wa Schalke kama anavyosema mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben ambaye alipachika mabao 3 jioni hiyo.

"Sifa zote zikiendee kikosi kizima cha Bayern. Tulicheza kwa kasi ya hali ya juu, na tulifanya vizuri sana. Hatukuwaruhusu Schalke kucheza kama wanavyotaka. Tulicheza kwa kasi kubwa, na kupachika mabao mengi. Hiki kilikuwa kipindi cha kwanza kizuri kwetu ambacho nimewahi kushuhudia."

Bayern sasa imekwenda michezo 20 ya nyumbani bila kufungwa ,na kushinda michezo 48 ya Bundesliga katika misimu miwili .

Bundesliga Fußball Bayer 04 Leverkusen vs. 1. FSV Mainz 05 Sami Hyypiae
Sami Hyypiä wa LeverkusenPicha: Alex Grimm/Bongarts/Getty Images

Katika msimamo wa ligi Bayern sasa imeweka pengo la points 20 kutoka timu inayoifuatia ambayo ni makamu bingwa wa msimu uliopita Borussia Dortmund ambayo ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya FC Nuremberg siku ya Jumamosi.

Bayer Leverkusen katika mzozo

Bayer Leverkusen iliyokuwa inashikilia nafasi ya pili imekumbwa na mkosi wa kukubali vipigo, baada ya wiki hii kusalim amri mbele ya Mainz 05 kwa bao 1-0. Kipigo hicho hata hivyo ni cha tano mfululizo, kipigo ambacho kimefungua majadiliano iwapo timu hiyo iendelee kupata mafunzo kutoka kwa kocha wake Sami Hyypiä.

Mkurugenzi wa spoti wa Leverkusen Rudi Voller amesema timu yake imepungukiwa hali ya wepesi wa kufanya mambo uwanjani.

Fußball Bundesliga 23. Spieltag Borussia Dortmund - 1. FC Nürnberg
Kikosi cha kocha Klopp cha Borussia DortmundPicha: picture-alliance/dpa

"Kwa sasa tunakosa kabisa ile hali ya wepesi wa kufanya mambo ambayo yanahitajika uwanjani. Hali hiyo tulikuwa nayo wakati fulani, lakini sasa haipo kabisa. Na hiyo ndio sababu ya msingi. Na ndio sababu hatuwezi kubadilisha lolote."

Baada ya kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Hamburg SV wiki iliyopita Dortmund ilibidi kufanya kweli dhidi ya FC Nuremberg timu ambayo katika mzunguko huu wa pili wa ligi ya Ujerumani wamekuwa wakifanya vizuri ambapo wamefungwa mara mbili tu, na Bayern Munich pamoja na Borussia Dortmund. Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp amezungumzia ushindi huo.

"Kwangu mimi, ni siku saba tu baada ya kuwepo kule Hamburg ambapo hali ya kufanya mambo kiurahisi uwanjani haikuonekana kabisa. Ukitaka kufanya kazi kwa urahisi ni lazima kuwapo na wakati wa kufanyakazi kwa wepesi. Lakini leo tumeweza kutekeleza kazi ngumu iliyotukabili."

Fußball Bundesliga 23. Spieltag Eintracht Frankfurt VfB Stuttgart
Wachezaji wa Stuttgart wakiwa wameduwaa baada ya kushindwa na FrankfurtPicha: Thorsten Wagner/Bongarts/Getty Images

Mpambano kati ya timu zinazowania kujitoa kutoka katika nafasi ya kushuka daraja kati ya Eintracht Frankfurt dhidi ya VFB Stuttgart ulimalizika kwa Frankfurt kupata ushindi wa mabao 2-1 licha ya Stuttgart kupata bao la kuongoza ambalo lilidumu hadi katika dakika ya 80 ya mchezo ambapo Jan Rosenthal alipachika bao la kusawazisha na dakika tisa baadaye Alexander Meier aliwalaza mapema Stuttgart.

Mvua ya magoli

Mvua ya magoli pia ilinyesha jana huko Hoffenheim wakati timu hiyo ilipoikaribisha nyumbani Wolfsburg na kuibugiza mabao 6-2.

Ulikuwa mchezo ambao mashabiki na wachezaji wa Wolfsburg wangependa kuusahau kabisa.

Wakati huo huo kocha wa eintracht Frankfurt Armin Veh ameamua kuwa hataifunza tena timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika, amesema mwenyekiti wa klabu hiyo kongwe Heribert Bruchhagen leo(03.03.2014).

Eintracht Frankfurt - VfB Stuttgart
Kocha Armin Veh wa FrankfurtPicha: picture-alliance/dpa

Amefanya kazi nzuri sana katika klabu hii kwa muda wa miaka mitatu. Tumejaribu kumshawishi kurefusha mkataba wake lakini hatukufanikiwa, ameongeza Bruchhagen wakati akizungumza na shirika la habari la DPA.

Pellegrini anyakua taji la kwanza

Wakati huo huo huko nchini Uingereza, baada ya kushuhudia ukame wa mafanikio kabla ya kuingia kwa fedha kutoka kwa tajiri kutoka Abu Dhabi mwaka 2008 , Manchester City imefanikiwa kupata taji lake la tatu ndani ya muda wa miaka mitatu jana Jumapili, baada ya timu hiyo kunyakua taji la kombe la ligi katika mchezo wa fainali dhidi ya Sunderland katika uwanja wa Wembley.

Pamoja na mchezo huo wa fainali lakini pia kulikuwa na michezo mitatu ya ligi ya Uingereza Premier League. Roberto Soldado alifunga bao lake la kwanza katika muda wa miezi miwili wakati Tottenham Hot Spurs iliyoko katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi ilipoishinda Cardiff kwa bao 1-0.

Aston Villa imejisogeza juu zaidi kutoka katika eneo la hatari ya kushuka daraja kwa kuishinda Norwich City kwa mabao 4-1. Norwich iko katika nafasi ya 15 katika nafasi kati ya Swansea City na Crystal Palace, timu ambazo zilitoshana sare ya bao 1-1.

Cristiano Ronaldo aliweka wavuni bao la kusawazisha wakati Real Madrid ikiepuka kipigo katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya mahasimu wao wakubwa Atletico Madrid na kumaliza mchezo huo kwa sare ya mabao 2-2 jana Jumapili.

Barcelona ilipunguza mwanya wa points kati yake na Real Madrid hadi point moja baada ya ushindi mnono jana wa mabao 4-1 dhidi ya vijana machachari wa Almeria ambao wako katika nafasi ya kushuka daraja msimu huu.

Cristiano Ronaldo
CR7 Cristiano RonaldoPicha: picture-alliance/dpa

Huko nchini Italia Juventus Turin ilidhihirisha ubabe wake katika ligi hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya AC Milan na kujisogeza points 11 mbele ya timu inayoifuatilia ya Roma. SSC Napoli iliyoko katika nafasi ya tatu ilikwenda sare ya bao 1-1 na Livorno.

Huko Ufaransa Paris St. German imeongeza uongozi wake dhidi ya Monaco katika msimamo wa ligi ya nchi hiyo hadi points nane baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Marseille.

Salomon Kalou alipachika mabao matatu wakati Lille ikiendelea kung'ang'ania katika nafasi ya tatu kwa ushindi wa mabo 3-2 dhidi ya Ajaccio.

Yanga na timu za Waarabu

Katika bara la Afrika Dar Young Africans ya Tanzania ilifanikiwa kwa mara ya kwanza kuuangusha mbuyu, baada ya timu hiyo kuishinda Al Ahly ya Misri kwa bao 1-0 nyumbani mjini Dar Es Salaam katika mchezo wa Champions League katika bara la Afrika.

Gor Mahia ya Kenya ikapata kipigo nyumbani cha mabao 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi Esperance kutoka Tunisia , na Astres ya mjini Duala Cameroon ikatoka sare ya bao 1-1 na TP Mazembe ya DRC.

Flambeau I'Est ya Burundi ikaiangusha Coton Sport ya Cameroon kwa bao 1-0 nyumbani , na Entente Setif ya Algeria ikaibugiza ASFA Yennenga ya Burundi kwa mabao 5-0. Stade Malien ya Mali ikatoka sare ya bila kufungana na Al-Hilal ya Sudan.

Nkana Red Devils ya Zambia ilitoka sare na Kampala City Coucil kwa kufungana mabao 2-2 mjini Ndola.

Pistorius kizimbani

Wakati huo huo kesi ya mauaji dhidi ya mwanariadha maarufu nchini Afrika kusini anayekimbia kwa miguu ya bandia ya chuma Oscar Pistorius imeanza rasmi mjini Pretoria.

Waendesha mashtaka wamemshitaki mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp na kudai yalikuwa ni mauaji ya kukusudia.

Oscar Pistorius Freundin Südafrika Gericht Schüsse Tod
Oscar Pistorius kizimbaniPicha: picture-alliance/dpa

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ametoa ushahidi leo kwamba alisikia kilio kabla ya kusikia milio minne ya bunduki usiku ambapo mwanariadha huyo alimuua mpenzi wake.

Mvuto mkubwa kwa umma wa Afrika kusini katika kesi hiyo umeoneshwa kuzinduliwa jana usiku kwa televisheni itakayoonekana kwa saa 24 na ambayo itakuwa inaonesha zaidi kesi hiyo mahakamani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman