Bayern haina mshindani katika Bundesliga
15 Januari 2018
Tuanze na Bundesliga: Borussia Dortmund ilitoka sare ya bila kufungana jana Jumapili na VFL Wolsburg, ambao ni vidume wa kutoka sare katika Bundesliga. Borussia Dortmund iliteremka dimbani jana bila jogoo wake mshambuliaji nyota Pierre-Emerick Aubameyang , ambaye aliondolewa katika kikosi hicho kwa mara nyingine tena kwa kushindwa kufika katika kikao cha timu. Kocha wa Borussia Dortmund Peter Stoeger amezungumzia kuhusu suala hilo na kusema.
"Mimi binafsi hiyo si kitu kwa kweli , ni lazima niseme. Tatizo ni kwamba kwangu mimi sielewi, kwa nini, kwa kuwa anafanya mazowezi vizuri tu, na siwezi kuwaambia hasa, kwa nini anafanya hivi mara nyingi. Nina uvumilivu vya kutosha. Najaribu mambo mengi kuyaweka sawa. Lakini nikijisikia kwamba , haiwezekani tena, nachukua uamuzi kama huo, lakini binafsi sijisikii vibaya. Kwanza kabisa namthamini sana pamoja na hayo. Lazima atakuwa na sababu, nina matumaini hayo, na namkubali. Nadhani hana matatizo.
Aubameyang ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, anatoa changamoto kwa uvumilivu wa Borussia Dortmund. Aliondolewa kutoka katika kikosi cha timu hiyo katika mchezo wa jana dhidi ya Wolfsburg kwa kukosa mkutano wa timu, na hatua ya Aubameyang kukiuka nidhamu kunafuatia kuondolewa pia katika kikosi mwezi Novemba kwa kupiga picha ya video ambayo hajaruhusiwa katika uwanja wa mazowezi wa klabu hiyo.
Pia aliondolewa kutoka katika kikosi hicho msimu uliopita kwa kusafiri kwenda Milan Italia muda mfupi kabla ya mchezo wa Champions League. Aubameyang mwenye umri wa miaka 28 amefumania nyavu mara 13 msimu huu katika michezo 15 ya ligi , huku kukiwa na ripoti za kutakiwa na klabu nchini China na pia Arsenal London.
Iwapo hataki kucheza hapa , tutampa nafasi yake mtu mwingine," amesema kocha wa Dortmund Peter Stoeger. Kuhusu mchezo wa jana dhidi ya Wolfsburg na kupoteza nafasi nyingi za wazi za kupata bao mlinda mlango wa Borussia Dortmund Roman Burki alisema.
"Ukiangalia mchezo wenyewe, nadhani , kila upande ulipata nafasi za kufunga. Nafikiri pia , tungeweza kupata nafasi nyingi zaidi , iwapo tungecheza vizuri zaidi na kushambulia hadi mwisho. Hilo tulipaswa kulifanya vizuri zaidi. Inasikitisha kwetu kwamba tumeambulia pointi moja tu."
Bundesliga yarejea uwanjani
Katika ufunguzi wa dimba la Bundesliga siku ya Ijumaa, Bayern Munich ilifanikiwa kutoa ishara kwa timu zote za Bundesliga kwamba mara hii tena wako njiani kulipeleka taji la Bundesliga mjini Munich na hali hiyo haitabadilika. Bayern Munich wakikaribishwa nyumbani na Bayer Leverkusen waliuteka uwanja wa Bay Arena kwa kuizaba Bayer Leverkusen bila taabu kwa mabao 3-1 kama ilivyokuwa katika mchezo wa kuanza ligi ya msimu huu 2017 /18.
Timu iliyotoka uwanjani na kicheko na kifua mbele zaidi wiki hii hata hivyo ilikuwa FC Kolon ambayo ilifanikiwa kwa mara ya pili msimu huu kupata pointi zote 3 baada ya kuwangusha Borussia Moenchengladbach kwa mabao 2-1 kwa bao safi la dakika za majeruhi la Simon Terodde aliyerejea hivi karibuni kutoka Wolfsburg alikoanzimwa.
FC Kolon imekusanya sasa pointi 9 ikiwa bado inashiklilia mkia lakini ushindi wa jana ni dalili ya kufufuka na kupambana kujiondoa kutoka katika hatari ya kushuka daraja. Huyu hapa mfungaji wa bao hilo muhimu la ushindi kwa FC Kolon Simon Terodde.
"Sina maneno ya kuelezea, Katika dakika za mwisho nilikuwa bila kujijua nilikimbilia karibu ya nguzo ya goli. ilikuwa ni krosi nzuri sana , nilipeleka mwili wangu kuelekea mpira, na kuupeleka katika nyavu ndogo, safi sana. Baada ya hapo sikukumbuka kitu tena chochote kilichotokea. Nafikiri , kulikuwa na watu kumi ama kumi na tano wako juu yangu. Ulikuwa ushindi muhimu sana leo."
Mario Gomez
Mchezaji wa kiungo wa Borussia Moenchengladbach Patrick Herrmann alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na kipigo hicho.
"Haieleweki kabisa. Ni mchezo wenye machungu sana , hatujawahi kushindwa namna hii. Hasa katika mchezo wa Derby katika dakika za mwisho tunafungwa bao na Kolon, inaumiza sana. na katika kipindi cha pili tulikuwa timu bora kabisa uwanjani , tulipata nafasi mbili, nzuri za kufunga na tulipaswa kushinda mchezo ule."
Stuttgart nayo ikimkaribisha kijana wao aliyerejea nyumbani Mario Gomez ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Hertha Berlin , kwa goli ambalo mlinzi wa Hertha Berlin Niklas Stack alijifunga mwenyewe.
Hannover ikairarua Mainz 05 kwa mabao 3-2.
RB Leipzig inashikilia hivi sasa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 31 wakifuatiwa na Schalke 04 yenye pointi 30 na Borussia Dortmund iko katika nafasi ya 4 ikiwa na pointi 29 , wakati Bayer Leverkusen na Borussia Moenchengladbach zinashikilia nafasi ya kucheza katika Europa League kwa sasa katika nafasi ya 5 na 6.
Werder Bremen kwa kutoka sare na Hoffenheim siku ya Jumamosi haikusogea mbali sana na eneo la hatari ya kushuka daraja , na iko nafasi ya 16, Hamburg SV ambayo miaka minne iliyopita imeendelea kusumbuka kujinasua kutoka kushuka daraja bado iko katika hatari hiyo msimu huu ikiwa na pointi 15 na katika nafasi ya 17.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape /
Mhariri: Yusuf , Saumu