Bayern hawajalishwi na chochote katika Bundesliga
27 Desemba 2013Kila msimu huleta sura mpya katika Bundesliga, lakini siyo kila msimu humleta mtu mwenye tajriba kubwa kama vile kocha wa Bayern Pep Guardiola. Fikra zozote kwamba Bayern wangekuwa na matatizo katika kuuzozea mchezo wa mwalimu wao wa kasi na pasi fupi maarufu kama Tiki-Taka zilitokomea mbali. Mabingwa hao watetezi hawajashindwa mechi hata moja na wameangusha point nne tu katika mechi zao 16 za Bundesliga. Ni vyema tuseme tu kuwa BAYERN tayari wamelitwaa taji la msimu huu hata kabla ya msimu kuingia katika duru ya mwisho.
Anafahamika sana kwa uzungumzaji wake, lakini Kocha Jurgen Klopp katika siku za karibuni hajakuwa na mahusiano mazuri na maafisa wa Bundesliga msimu huu. Mara nyingi alionekana kuwa mwenye hasira za mkizi wakati mechi zikiendelea uwanjani, na hasa mchuano wa Champions League ambapo alipigwa marufuku mechi mbili.
Hata hivyo idadi ya majeruhi ambayo yamekiathiri kikosi cha Dortmund, na hata wakati mmoja mabeki wote wanne wakawa mkekani, yamemkosesha usingizi. Dortmund wataanza mwaka mmpya wakiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Borussia Moenchengladbach ambao waliwaruka Dortmund hadi nafasi ya tatu, katika mechi ya mwisho ya mwaka wa 2013, ndio waliowashangaza wengi katika nusu ya kwanza ya msimu. Na mmoja wa wachezaji waliong'ara ni Raffael ambaye magoli yake tisa yamemfanya kuwa mchezaji wa kiungo aliyefunga magoli mengi Ujerumani.
Timu inayomfanya kila mtu kuendelea kukisia ni Bayer Leverkusen, ambao wamejisukuma katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, hatua nyingi nyuma ya Bayern lakini na pengo zuri la point nne mbele ya Gladbach.
Ila ukimuuliza mtazamaji yeyote wa Bundesliga akutajie mchuano uliowahi kumfurahisha wa Leverkusen, atakwambia tu hajui. Lakini ukimuuliza ni upi mbaya zaidi, atakwambia kichapo walichopewa na washika mkia Braunschweig, au kile cha magoli matano kwa sifuri dhidi ya Manchester United katika Champions League. Hivyo mbona wako katika nafasi ya pili? Huednani ufungaji mabao wa mshambuliaji wao Stefan Kiessling au miujiza ya kipa wao Bernd Leno..au mbinu za kiufundi za kocha wao Sammi Hyppia. Tutasubiri kuona katika mkondo wa lala salama jinsi mambo yatakavyowaendea.
Nuremberg imeweka rekodi ya kuwa klabu pekee ambayo haijashinda mchuano hata mmoja katika nusu ya kwanza ya msimu. Na kwa sasa wanashikilia mkia pamoja na Eintrahcht Braunschweig.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman