1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern washika bendera ya Bundesliga

11 Machi 2019

Bayern Munich wameushika uongozi wa Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga kwa kishindo, baada ya kuwalaza VfL Wolfsburg magoli sita kwa bila katika uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena siku ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/3EnG1
Bundesliga FC Bayern München v VfL Wolfsburg | Jubel
Picha: Reuters/M. Dalder

Walipokuwa wakiingia katika mechi hiyo, Bayern walikuwa sawa kipointi na Borussia Dortmund ila tofauti ya mabao ndiyo iliyowatenganisha. Wachezaji wote watatu Jerome Boateng, Thomas Müller na Mats Hummels ambao kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw mwanzoni mwa wiki alisema kwamba hatohitaji tena huduma zao katika timu ya taifa, walikuwa katika kikosi cha kwanza cha Bayern katika mchuano huo. Robert Lewandowski alifunga mabao mawili kisha Thomas Müller, Joshua Kimmich, James Rodriguez na Serge Gnabry wakapata bao moja kila mmoja. Kocha wa Wolfsburg Bruno Labbadia alikuwa na haya ya kusema baada ya mechi hiyo.

Dortmund waliwaza Stuttgart Signal Iduna Park

"Unaweza kuona kwamba Bayern wametumia vizuri nafasi yao baada ya Dortmund kuteteleka, wamepita kipindi chao kigumu kwa haraka na ukiangalia hata mechi yao ya Champions League, walicheza vizuri dhidi ya Liverpool na unaweza kusema kwamba Bayern ni miongoni mwa timu zinazoweza kuebuka na ubingwa na hata kwenye ligi ya Ujerumani," alisema Labbadia.

Bundesliga Borussia Dortmund v VfB Stuttgart | Jubel Pulisic
Christian Pulisic akisherehekea baada ya kufunga bao la tatuPicha: Reuters/W. Rattay

Borussia Dortmund walikuwa wanacheza na Stuttgart katika uwanja wao wa nyumbani Signal Iduna Park na waliebuka washindi wa magoli matatu kwa mawili, Marco Reus, Paco Alcacer na Christian Pulisic wakiwa wafungaji wa magoli hayo huku Stuttgart wakifungiwa na mabao yote mawili na Marc Oliver Kempf. Kwa sasa Dortmund wako sawa na Bayern Munich wote wakiwa na pointi hamsini na sana ila Bayern wanaongoza kutokana na wingi wa mabao mawili.

Mechi zengine za Bundesliga zilishuhudia Leipzig kutoka sare ya kutofungana na Augsburg kisha Freiburg wakawalaza Herth BSC Berlin mbili moja na Borussia Mönchengladbach wakaebuka kidedea moja bila dhidi ya Mainz. Hoffenheim walikuwa wanacheza na Nurnberg na walishinda mbili moja kisha Bayer Leverkusen waliokuwa ugenini wakicheza na Hannover walipata bahati ya kuponyoka na alama zote tatu walipowalaza wenyeji wao mabao matatu kwa mawili katika mechi ambayo ilisimamishwa kwa muda kutokana na theluji nyingi iliyokuwa inadondoka, kisha shuti la Genki Haraguchi alilokuwa amelipiga baada ya kumchenga mlinda lango wa Leverkusen, likashindwa kuingia wavuni kutokana na theluji iliyokuwa nyingi uwanjani.