Bayern mabingwa tena Bundesliga
9 Aprili 2018Bayern Munich imetia kibindoni taji lake la 28 la Bundesliga wiki hii baada ya kutawazwa tena kwa mara ya sita mfululizo kuwa mabingwa siku ya Jumamosi baada ya kuikandika Augsburg kwa mabao 4-1. Bayern imedhihirisha kwamba wao ni washindi wasioshindia katika Bundesliga.
Sherehe za Bayern hata hivyo zilionekana kuwa katika hatari ama kucheleweshwa wakati mlinzi wao Niklas Sulle alipouweka mpira katika wavu wake. Hata hivyo Corentin Tolisso na James Rodriguez walipachika mabao ya haraka kwa mabingwa hao kabla ya mapumziko na kisha Arjen Roben na Sandro Wagner walimalizia katika kipindi cha pili.
Bayern ambayo ina pointi 72 kutoka michezo 29 ya bundesliga msimu huu, imefungua mwanya wa pointi 20 kutoka timu iliyoko nafasi ya pili Schalke 04, ambayo ilipokea kipigo bila kutarajiwa cha mabao 3-2 dhidi ya timu iliyoko mkiano ya Hamburg SV.
Ilikuwa ni mafanikio makubwa ya binafsi kwa kocha mwenye umri wa miaka 72 wa Bayern Jupp Heynckes , ambaye alitoka katika kustaafu mwezi Oktoba na kuchukua nafasi ya Carlo Ancelotti akirejea mara ya nne katika klabu ya Bayern wakati timu hiyo ikiwa nyuma kwa pointi tano dhidi ya Borussia Dortmund.
„Nilikuwa na imani kwamba, tunaweza kubadilisha mambo. Ilikuwa katika wakati huu Borussia Dortmund ikiongoza kwa pointi 5 na ilicheza vizuri sana. Na ndio sababu watu hawakudhani kwamba , hivi sasa tungekuwa mabingwa wa Ujerumani. Tumepiga hatua kubwa sana. Hata mimi binafsi sikufikiria hivyo, badala yake kwangu ilikuwa wazi , kwamba tujiimarishe tu pale tulipo."
Licha ya kwamba sherehe za ubingwa hazikuwa kama miaka yote, kutokana na majukumu mengine kama ya champions league na kombe la shirikisho nchini Ujerumani DFB, lakini wachezaji waliruka ruka uwanjani mjini Augsburg kuashiria kwamba bado wana uchu wa kunyakua mataji mengi zaidi. Arjen Robben aliyefunga bao alikuwa na haya ya kusema.
„Ubingwa ni ubingwa tu. Tumeshuhudia baada ya kubadilisha kocha tulikuwa pointi 5 nyuma ya Borussia Dortmund. Na nasema kila wakati, kila mtu anasema Bayern ina kikosi kizuri sana, msimu huu tumekwenda mbali zaidi, na hili linaeleza kila kitu. Lakini kile ambacho mtu hapaswi kusahau ni kwamba katika Bundesliga hupati matokeo kama zawadi kwa kuwa tunafanyia kazi. Wakati ukiwa huko vizuri kimchezo, huna umakini huwezi pia kushinda mchezo."
Hamburg ambayo imekuwa katika historia ya miaka 55 ya ligi ya Ujerumani Bundesliga , imesogea juu kidogo mwishoni mwa juma hili kutoka mkiano kabisa mwa ligi na kujipa matumaini madogo ya kujinasua kutoka kushuka daraja wakati ilipoishinda Schalke 04 kwa mabao 3-2.
Timu nyingine iliyoko mkiani mwa ligi FC Kolon ilikuwa na matumaini ya kutoroka na pointi zote tatu katika uwanja wake siku ya Jumamosi ilipotiana kifuani na Mainz 05, ikiwa na matumaini ya kujiongezea pointi na hatimaye kujinasua kutoka katika hatari ya kushuka daraja matumaini hayo yaliishia ukingoni baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo mkali nyumbani siku ya Jumamosi.
Borussia Dortmund baada ya kubugizwa mabao 6-0 na mabingwa Bayern Munich wiki iliyopita, ilikuwa bado katika fadhaa ya aibu hiyo kubwa iliyowakuta msimu huu. Na baada ya kubabaika katika kipindi cha kwanza walijikongoja na kupata ushindi usioridhisha wa mabao 3-0 dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu ya VFB Stuttgart.
Bado Dortmund haijathibitisha hadhi yake ya kuwa nguvu ya pili mbadala katika Bundesliga baada ya Bayern na msimu huu imesuasua licha ya kupata ushindi hapa na pale bila kuthibitisha kwa mchezo safi ambao umekonga nyoyo za mashabiki wa kandanda duniani.
Borussia Moenchengladbach ilifanikiwa kubadilisha matokeo kutoka kuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Hertha Berlin na kupata ushindi muhimu wa mabao 2-1 licha ya mashabiki wa timu hiyo kulalamikia uchezaji wa timu hiyo na jinsi walivyopata ushindi. Baada ya kuwa sare kwa bao 1-1, ghafla mwamuzi Bibiana Steinhous aliombwa kuangalia vidio kutoka kwa mwamuzi wa vidio na kuurejesha mpira katika eneo la adhabu la Hertha Berlin na kuwa penati ambayo Thorgan Harzad aliuweka wavuni na kuwa bao la ushindi kwa Moenchengladbach.
Ushindi huo hata hivyo haukuwafurahisha mashabiki wake. Kocha Dieter Hecking hata hivyo alisema amefurahishwa na ushindi huo licha ya kucheza chini ya kiwango.
„Uwezo wetu katika kipindi cha kwanza haukufikia kiwango kinachotakiwa. Kila mtu uwanjani aliliona hilo. Tulijiingiza katika matatizo makubwa katika ujenzi wa mashambulizi yetu. Ilionekana kwamba hatukuwa makini , licha ya kuwa tulitaka kucheza kwa haraka zaidi. Hertha walitubana sana. Tulikuwa na matatizo, ambayo baada ya kufungwa bao, tungepaswa kujilinda vizuri zaidi, licha ya kwamba tuko nyuma. Ilikuwa wazi wakati wa mapumziko, kwamba hatukuwa na hamasa na tuliwaambia, vijana jaribuni kwa njia yoyote ile kubadilisha matokeo. Tuliweza kweli kubadilisha matokeo. Ilikuwa hali ya kuonesha dhamira , licha ya kuwa hatukuonesha mchezo wa hali ya juu."
Leo Bundesliga inakamilisha mchezo wake wa 29 ambapo RB Leipzig inaikaribisha Bayer Leverkusen, timu ambazo ziko katika nafasi ya 5 na 6 zikipishana kwa pointi moja.
Wakati tunawapongeza Bayern Munich kwa ushindi wa taji lao la sita la Bundesliga mfululizo , sasa mtazamo unaelekea katika timu kuwania kucheza katika Champions League na pia kujinasua kutoka katika hatari ya kushuka daraja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga