1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich bado kiboko katika Bundesliga

10 Februari 2014

Bayern Munich bado haina mshindani katika Bundesliga,Hamburg yatumbukia zaidi katika mzozo na hatari ya kushuka daraja, wakati VFB Stuttgart nayo haijaonja ushindi katika michezo mitano ya ligi mfululizo.

https://p.dw.com/p/1B6K3
Fußball Bundesliga FC Bayern FC Nürnberg 08.02.2014
Wachezaji wa Bayern wakishangiria baoPicha: Christof Stache/AFP/Getty Images

Na huko Sochi medali zaanza kumiminika Norway yaongoza.

Mdudu gani ananuka katika kambi ya VFB Stuttgart? Mashabiki wa soka wanajiuliza. Baada ya kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya FC Augsburg , Stuttgart sasa inajikuta katika nafasi ya kushuka daraja, ambapo katika wiki zinazokuja inajikuta katika hali ya hatari zaidi baada ya mshambuliaji wao hatari Vedad Ibisevic , kuoneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa jana na atakosa michezo kadha ijayo.

VfB Stuttgart - FC Augsburg
Vedad Ibisevic akioneshwa kadi nyekunduPicha: picture-alliance/dpa

Mkurugenzi wa spoti wa Stuttgart Fredi Bobic amesema timu yake ilikosa bahati kabisa.

"Ni matokeo yasiyokuwa na shaka, ni matokeo machungu kwa kweli. Na hata idadi ya mabao inaonesha udhaifu tuliokuwa nao, licha ya kuanza vizuri mchezo huu, ambapo katika dakika 30 kila kitu kilikuwa kinakwenda vizuri, lakini kosa dogo lilibadilisha kila kitu na tukajikuta katika hali ngumu."

Jana jioni(09.02.2014) katika mchezo mwingine wa Bundesliga Schalke 04 ilijinyakulia points zote tatu dhidi ya Hannover 96, timu iliyoanza vizuri mzunguko wa pili wa Bundesliga kwa ushindi mara mbili. Schalke ilitoka uwanja ikiwa kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0.

Bundesliga Hannover Schalke 04 09.02.2014
Schalke 04 wakishangiria bao dhidi ya HannoverPicha: picture-alliance/dpa

Bayern Munich imeonesha kuwa haina mshindani msimu huu, baada ya siku ya Jumamosi kudhihirisha kwa mara nyingine tena ubabe wake dhidi ya Nürnberg katika pambano la watani wa jadi, ambapo Bayern iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0. Hapo kabla makamu bingwa wa Bundesliga Borussia Dortmund ilipata ushindi wake wa kwanza mnono mwaka huu kwa kuirarua Werder Bremen kwa mabao 5-1.

Mgogoro Hamburg

Mgogoro mkubwa hata hivyo umeikumba Hamburg SV , timu ambayo imekuwamo katika Bundesliga tangu ilipoanzishwa mwaka 1963 , na kutimiza misimu 51 mwaka huu. Hamburg SV imejikuta ikichezea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Hertha BSC Berlin.

Fußball Bundesliga HSV Hertha BSC 08.02.2014
Nahodha wa Hamburg van der Vaat haamini kinachotokeaPicha: picture-alliance/dpa

Bodi ya wakurugenzi ya Hamburg SV ilimaliza kikao chake cha saa nane jana Jumapili bila ya kufikia uamuzi juu ya hali ya baadaye ya uongozi wa klabu hiyo kongwe baada ya kipigo cha sita mfululizo.

Jana Jumapili , bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo ilimwita rais wa klabu Carl Jarchow na mkurugenzi wa spoti Oliver Kreuzer na kuwahoji kwa muda wa dakika 75 katika hoteli ya Grand Elysee, na ilibidi watokee mlango wa uwani kurejea makawao.

Fußball Bundesliga HSV Hertha BSC 08.02.2014
Wachezaji wa Hertha wakifurahia bao la pili la Adrian RamosPicha: Oliver Hardt/Bongarts/Getty Images

Siku ya Jumamosi baada ya kipigo dhidi ya Hertha , mashabiki wenye hasira waliwashambulia wachezaji na kudai rais wa klabu hiyo Carl Jarchow ajiuzulu.

Chelsea yapeta

Kwingineko katika ligi za Ulaya Chelsea imechukua usukani wa ligi ya Uingereza Premier League kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Newcastle United , wakati Arsenal London inayoshika nafasi ya pili sasa ilibugia mabao 5-1 dhidi ya Liverpool, ambapo Manchester City iliridhika na sare ya bila kufungana dhidi ya Norwich City.

Lakini bado mdudu wa kunuka yuko katika kambi ya Manchester United ambapo kikosi hicho cha David Moyes hakikuwa na jibu sahihi katika mchezo wake dhidi ya Fulham na kutoka sare ya mabao 2-2 ndani ya nyumba, Old Trafford.

FC Everton Trainer David Moyes
David Moyes kocha wa Manchester UnitedPicha: Getty Images

Katika ligi ya Uhispania , La Liga , Lionel Messi alifunga mabao safi mawili wakati Barcelona ikirejea kileleni mwa ligi hiyo kwa ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Sevilla. Atletico Madrid ilionja joto ya jiwe kwa kukandikwa mabao 2-0 na Aleria , wakati Real Madrid ilipita bila kizuwizi dhidi ya Villareal kwa ushindi wa mabao 4-2.

Nchini Italia Carlos Tevez aliifungia timu yake ya Juventus mabao mawili lakini hayakutosha kuipa ushindi timu hiyo wakati Verona ilirejesha mabao hayo na kulazimisha sare ya mabao 2-2. Napoli ikiwa ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo Serie A ilikirarua kikosi cha Clarence Seerdorf , AC Milan kwa mabao 3-1.

Carlos Tevez
Carlos Tevez wa Juventus TurinPicha: APImages

Na ule mchezo uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa wa watani wa jadi kati ya viongozi wa ligi ya Ureno Benfica Lisbon na Sporting iliyoko katika nafasi ya tatu uliahirishwa na mashabiki wakaondolewa uwanjani , baada ya kutokea upepo mkali uliosababisha paa la uwanja huo kuvunjika , uwanja ambao utafanyika fainali ya msimu huu ya kombe la mabingwa wa Ulaya Champions League.

Kombe la shirikisho

Wakati huo huo kesho Jumanne inaanza michezo ya robo fainali ya kombe la shirikisho la Ujerumani DFB Pokal , ambapo Eintracht Frankfurt inaikaribisha nyumbani Borussia Dortmund. Borussia haitakuwa na wachezaji wake muhimu kama Marco Reus na Sven Bender ambao ni majeruhi, pamoja na Mats Hummels ambaye alipata maumivu katika mchezo wa majaribio wiki iliyopita.

Siku ya Jumatano itakuwa zamu ya Hamburg SV ikiikaribisha Bayern Munich , Bayer Leverkusen itakwaana na Kaiserslautern ya daraja la pili na Hoffenheim inaikaribisha Wolfsburg.

Huko Uhispania Barcelona inaweza kukata tikiti yake katika fainali ya kombe la mfalme , Kings Cup , Copa del Rey wiki hii kabla ya kuelekeza mawazo yao katika Champions League.

Barca inakwaana na Real Sociedad siku ya Jumatano ambapo inaingia katika mchezo huo ikiwa mbele kwa mabao 2-0 kutoka katika mchezo wa kwanza. Real Madrid inakwenda ugenini kupimana ubavu na Atletico Madrid kesho Jumaane, ambapo inaongoza pia kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza.

Huko mjini Sao Paulo nchini Brazil maafisa wamesema kuwa mashabiki watatu wamejeruhiwa katika shambulizi la risasi baada ya mchezo uliofanyika katika uwanja utakaofanyika michuano ya fainali za kombe la dunia nchini Brazil mwishoni mwa juma. Mashabiki hao hata hivyo hawako katika hali mbaya ya maisha yao.

Mabingwa wa Afrika

Ligi ya mabingwa barani Afrika ilianza rasmi mwishoni mwa juma hili na mabingwa wa Tanzania Dar Young Africans iliiadhibu Komorozine ya visiwa vya Comoro kwa mabao 7-0 mjini Dar Es Salaam wakati KMKM ya Zanzibar ilisalim amri mbele ya Dedebit ya Ethiopia kwa kipigo cha mabao 3-0.

Mjini Nairobi Gor Mahia ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya AS Bitam ya Gabon , wakati Kampala City Council iliibuka kidedea dhidi ya Al Merreikh ya Sudan kwa ushindi wa mabao 2-0 nyumbani. Rayon Sport ya Rwanda ikatoka sare ya bila kufungana na AC Leopards ya Congo na AS Vita Club ya DRC ikaikung'uta Kano Pillers ya Nigeria kwa mabao 3-1.

Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi

Na katika michezo ya olimpiki ya Sochi, kamati ya kimataifa ya Olimpiki imewakaripia wanariadha kwa kuvaa jezi zenye ujumbe wa kukumbuku ya watu waliofariki. Msemaji wa IOC Mark Adams amesema leo kuwa kamati ya olimpiki imetuma barua katika kamati ya olimpiki ya Norway baada ya mwanariadha wake wa mbio za kuteleza katika barafu kuvaa kitambaa cheusi siku ya Jumamosi akimkumbuka mchezaji mwenzake ambaye ni kaka yake, aliyefariki katika mkesha wa michezo ya Sochi.

Sotschi 2014 - Biathlon
Mkimbiaji katika barafu wa Ujerumani katika michezo ya SochiPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo Norway inaongoza msimamo wa medali katika michezo hiyo ya olimpiki ya Sochi ya majira ya baridi kwa kuwa na jumla ya medali 7 , mbili za dhahabu, moja ya fedhja na nne za shaba. Inafuatiwa na Uholanzi yenye jumla ya medali 4 , mbili ziikiwa za dhahabu. Ujerumani iko nafasi ya 5 ikiwa na medali mbili za dhahabu.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / ape

Mhariri: Yusuf , Saumu