Bayern Munich bado kidume katika Bundesliga
1 Februari 2016Mabingwa watetezi Bayern Munich wameendelea kuchanja mbuga kuelekea ubingwa wao wa nne mfululizo wa Bundesliga , jana baada ya kuiagusha Hoffenheim kwa mabao 2-0.
Mshambuliaji wa Bayern kutoka Poland Robert Lewandowski ndie aliyepachika mabao hayo mawili na kufikisha mabao 19 katika Bundesliga msimu huu , akimfukuzia mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre Emerick Aubameyang ambaye hapo siku ya Jumamoyi nae alipachika mabao 2 na kuipa ushindi timu yake dhidi ya Ingolstadt iliyopanda daraja msimu huu. Aubameyang ana mabao 20 hadi sasa.
Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge alizungumzia kuhusu ushindi wa Bayern dhidi ya Hoffenheim jana.
"Kwa miaka michache iliyopita mara kadhaa tumeshindwa na Moenchengladbach katika mchezo wa kwanza , mwaka jana tulifungwa mabao 4-1 na Wolfburg. Msimu huu tumeshinda michezo yetu yote ya kwanza. Tumeshinda michezo yote miwili na kuendelea kuongoza ligi. Kila kitu ni kizuri."
Berlin yajiimarisha
Hertha BSC Berlin imejiimarisha katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Werder Bremen, wakati Leverkusen imepanda hadi nafasi ya nne baada ya kuchapa Hannover kwa mabao 3-0 siku ya Jumamosi.
Schalke 04 nayo imesogea juu kidogo hadi nafasi ya tano baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Damstadt siku ya Jumamosi. Lakini Wolfsburg imeendelea kubaki katika nafasi ya 7 baada ya kutoka sare jana Jumapili ya bao 1-1 dhidi ya FC Cologne.
Mchezaji wa kati wa Wolfsburg Julian Draxler amesema walitaka pointi zote tatu lakini hali haikuwa hivyo.
"Tulitaka pointi zote tatu iwapo goli letu lingesalia la ushindi. Bahati mbaya hali haikuwa hivyo leo, kwamba hatukuweza kuondoka na pointi hizo tatu. Ni kazi ya ziada tu ndio itatuwezesha kufanikiwa, tunapaswa kuendelea kupambana, na kuweza kupata mafanikio. wakati tukiwa katika hali kama hii , kila hatua ni muhimu tutakayopiga, ili kuweza kutoka chini tuliko. mafanikio bado hatujayapata, lakini inabidi kufanyia kati kupata pointi kwa vyovyote vile."
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga