Bayern Munich mabingwa wa Bundesliga
9 Mei 2016Bayern Munich imefanikiwa kunyakua ubingwa wake wa nne mfululizo katika Bundesliga baada ya kuichapa Ingolstadt kwa mabao 2-1 siku ya Jumamosi. Lakini furaha ya Bayern haikuwa kubwa hivyo baada ya kutolewa katika kinyang'anyiro cha Champions League katikati ya wiki dhidi ya Atletico Madrid.
Nahodha wa Bayern Philip Lahm amesema lengo lilikuwa kutwaa ubingwa tangu msimu ulipoanza.
"Ilikuwa lengo letu mwanzoni mwa msimu kuwa mabingwa. Ubingwa miaka minne mfululizo, haijawahi kutokea katika Bundesliga na hii ilikuwa ni chachu kubwa. Haikuwa rahisi kufanya hivyo, kwasababu Dortmund imekuwa na msimu mzuri sana na hivyo kutuweka katika mbinyo mkubwa, ilibidi kupata pointi kila mara. Na hii imekifanya kikosi chetu kucheza kwa umahiri mkubwa, na kuweka rekodi mpya."
Borussia Dortmund ambayo inashikilia nafasi ya pili katika Bundesliga, ambayo itakabiliana na Bayern katika kombe la shirikisho DFB Pokal Mei 21, ilipoteza mchezo wake kwa kufungwa bao 1-0 na Eintracht Frankfurt ambayo kwa ushindi huo Frankfurt imejiweka katika nafasi nzuri ya kujinasua katika hatari ya kushuka daraja.
Borussia Moenchengladbach inakaribia kabisa kunyakua nafasi ya nne ambayo itawawezesha kucheza katika Champions League katika michezo ya mchujo baada ya kuibwaga Bayer Leverkusena kwa mabao 2-1.
Werder Bremen na VFB Stuttgart huenda vikaifuata Hannover 96 katika njia ya kuelekea daraja la pili msimu ujao wakati kumebakia mchezo mmoja , baada ya siku ya Jumamosi Stuttgart kuangukia pua kwa kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Mainz 05. Hali hiyo inaiweka Stuttgart kutegemea miujiza kuweza kutoka katika nafasi hiyo na angalau kupata nafasi ya mchujo ambayo Werder Bremen imeishikilia hivi sasa ikiwa na pointi 35 dhidi ya 33 za Stuttgart.
Mlinzi wa Stuttgart Kevin Grosskreutz amesema. "Wote tunawajibika kwa hili na mimi pia. Nimefanya makosa leo na kila mmoja wetu. Na timu yetu inawajibika, kwa kile mashabiki wetu walichokifanya. Matumaini bado yapo, bado tuna mchezo mmoja na tunaweza kupata nafasi ya mchujo na hilo tutajaribu kulifanikisha. Tunapaswa katika mchezo wa mwisho kujitolea kwa kila hali."
Mpambano wa kuwania kujinasua kushuka daraja umeshika kasi mno wakati Hannover 96 imekwisha kata tamaa na inaelekea daraja la pili , lakini mchezo wa mwisho utaamua timu gani itashuka pamoja na Hannover siku ya Jumamosi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi sessanga