Bayern munich sasa yaongoza Bundesliga
5 Machi 2010Katika Premier League-Arsenal inaumana na Burnley, huku Manchester United ikitembelea Wanderes.Baada ya mapambano ya kati ya wiki ya kujiandaa kwa Kombe lijalo la dunia Juni hii nchini Afrika Kusini, ni timu za kanda gani zilizotamba :Amerika kusini au Ulaya baada ya Brazil kuitoa Ireland kwa mabao 2:0 na Argentina kuipiga kumbo Ujerumani mjini Munich kwa bao 1:0 ?
Ringi ya mabondia iwazi hapo Mei kwa mbabe wa wezani wa juu wa WBC, Vitali Klitchko wa Ukraine, akipewa changamoto na mbabe wa zamani, Nikolay Valuev wa Russia.
BUNDESLIGA:
Tukianza na Bundesliga, Bayern Munich inaongoza ligi hii kwa pointi mbili baada ya kuipiku Bayer Leverkusen na kuchukua uongozi kwa mara ya kwanza msimu huu. Leverkusen iliteleza nyumbani ilipocheza Jumamosi iliopita na mahasimu wao wa mtaani FC Cologne:Kesho Leverkusen ina miadi na Nüremberg wakati Munich leo Jumamosi inapambana na FC Cologne.
RAIS WA FIFA AZURU COMORO:
Afrika Kusini, mwenyeji wa Kombe la kwanza kabisa la dunia hapo Juni 11 mwaka huu, pale wenyeji Bafana Bafana watakapofungua dimba na Mexico, walianza kuhesabu siku 100 hadi siku hiyo wakiwa pamoja na rais wa FIFA, Sepp Blatter, aliyeondoa shaka shaka zozote zilizokuwapo juu ya uwezo wa Afrika Kusini kuandaa Kombe la dunia.
Baadae, Rais wa FIFA, Sepp Blatter, alitembelea visiwa jirani na Afrika Kusini, visiwa vya Comoro. Huko,Sepp Blatter, alipokewa na rais Sambi wa Comoro .Akatembelea uwanja wa dimba wa Mitsamiouli uliojengwa kwa msaada wa FIFA. Blatter akaiahidi Comoro msaada wa chuo cha michezo kabla hakurejea Afrika kusini.
2010:
Timu za Ulaya zilizojinoa kati ya wiki hii kwa Kombe lijalo la dunia huko Afrika Kusini, ili kutoroka na Kombe hilo,nyingine zilipata pig. Mabingwa wa Ulaya,Spian,walitamba mble ya makamo-bingwa wa dunia-Ufaransa, walipowachapa jirani zao mabao 2:0 na kutia mfukoni ushindi wao wa kwanza mbele ya wafaransa tangu kupita miaka 42. Hii iliwachochea mashabiki wa nyumbani Ufaransa, kurudi kupaza sauti kutaka kocha wa Ufaransa, Raymond Domenech, afunge virago vyake.
Mabingwa wa dunia-Italy walibanwa 0:0 na Simba wa nyika,Kameroun, huko Monte Carlo katika mchezo usiochangamsha, huku Uingereza, baada ya kujikuta iko nyuma kwa bao 1, waliwaambia mafiraouni, mabingwa wa Afrika, Misri, kutangulia si kufika. Ilikua Mohamed Zedane, anaecheza katika Bundesliga alielifumania lango la England uwanjani Wembley. Kocha Fabio Capello, akamuita uwanjani Twiga wake, Peter Crouch, na hakukawia kuchungulia ndani ya wavu wa Misri. Crouch, alilifumania lango la Misri mara mbili ili kukamilisha ushindi wa mabao 3:1 dhidi ya firaouni ambao hawakufuzu kwa Kombe lijalo la dunia huko Afrika kusini.
Ujerumani, mabingwa mara tatu, walisangazwa na chipukizi wa Diego Maradona katika uwanja wa Allianz Arena, mjini Munich. Argentina iliifedhehesha Ujerumani baada ya kipa wao, Rene Adler, kufanya madhambi ya kutoka nje ya goli lao kuokoa. Sasa hatima ya kocha wa Ujerumani, Joachim Loew, haijulikani, kwani, mkataba wake haujarefushwa.
Holland,ambayo haikuwahi kuvaa taji la dunia kama Spain, haikuwa na taabu kutamba kwa mabao 2-1 nyumbani mbele ya Marekani.
Wenyeji, Afrika Kusini, walimudu sare ya bao 1:1 na jirani Namibia na kwa kweli Bafana Bafana walitoka nyuma kusawazisha. Wakati Algeria ilifumaniwa nyumbani kwa mabao 3-0 na Serbia, na Ghana ikakomewa mabao 2-1 na Bosnia, Tembo wa Ivory Coast walionesha nao bado wanaugua maradhi walioyapata walipopigwa kumbo nje ya robo finali ya kombe la Afrika la mataifa. Walikandikwa mabao 2:0 na Korea ya Kusini mjini London.
Ni Nigeria tu iliotamba kwa mabao 5-2 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Senegal haikufuzu mara hii kwa kombe la dunia na hawatakuwa na nafasi ya kurejea ushindi wao wa 2002 huko Asia, walipoitoa Ufaransa. Hata hivyo, Senegal imeichezesha kindumbwe-ndumbwe Ugiriki kwa kuwakomea mabingwa hao wa Ulaya mwaka 2004 mabao 2:0.
Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE
Uhariri: Miraji Othman