1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich wafungua mwanya mpana Bundesliga

25 Januari 2021

Robert Lewandowski na Thomas Müller walikuwa miongoni mwa wafungaji katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga ambayo Bayern Munich waliebuka washindi wa magoli 4-0 dhidi ya Schalke hapo Jumapili.

https://p.dw.com/p/3oNtV
Fußball Bundesliga Schalke 04 v Bayern München | Tor 0:2 Lewandowski
Picha: Ina Fassbender/AFP

Ushindi huu umeupanua mwanya kati yao na timu iliyo katika nafasi ya pili RB Leipzig na sasa ni tofauti ya pointi saba kati yao huku mabingwa hao wakiwa na pointi 42 kutokana na mechi 18 na wakiwa kwa ujumla wamefunga mabao 53.

Bundesliga | FSV Mainz 05 - RB Leipzig
RB Leipzig wakicheza na MainzPicha: Kai Pfaffenbach/AFP/Getty Images

Bado kuna mengi ya kurekebishwa Bayern Munich

Huyu hapa kocha wa Munich Hansi Flick.

"Nafikiri kuna mambo mengi ambayo bado tunaweza kuyarekebisha. Katika kial mechi tunastahili kuonyesha mawazo yetu na bila shaka ushirikiano mwema. Mara kwa mara tulikuwa hatuna kasi ya mchezo na tulifanya mambo kuwa magumu na kisha mpira tukaupoteza. Hayo ndiyo mambo tunayoweza kurekebisha. Lakini nafikiri kama vile msimu uliopita ulivyoonyesha kwamba kila ushindi tunaopata, tunazidi kujiamini na tunazidi kuwa imara na kwasababu hiyo tunataraji kwamba tutakuwa na mwelekeo huo katika mechi zijazo," alisema Flick.

Leipzig wao walitetereka hapo Jumamosi walipozabwa 3-2 na vibonde Mainz na Bayer Lervekusen ambayo ndiyo timu inayoishikilia nafasi ya tatu ilinyukwa moja bila nyumbani kwao Bay Arena walipokuwa wakichuana na VfL Wolfsburg ambao kwa sasa wako sawa kialama na hao Leverkusen.

FC Cologne ilipoteza nafasi chungunzima

FC Cologne ambayo ni ya tatu kutoka mkiani, ilipokea kichapo cha magoli matatu bila jawabu ilipokuwa ugenini ikicheza na Hoffenheim. Andrej Kramaric alifunga mikwaju miwili ya penalti naye Christoph Baumgartner akaongeza la tatu .

Dominick Drexler ni kiungo mshambuliaji wa FC Cologne.

"Timu inapopoteza mechi kwa kukubali magoli matatu langoni, mawili kupitia mkwaju wa penalti na moja kwa kona, basi naamini inabidi tuanze kujiangalia upya kwasababu haikubaliki. Sisi wenyewe tulipata mkwaju wa penalti, tuligonga na nafasi nyengine ya kufunga tukagonga mwamba na pia nafasi nzuri ya Marius Wolf kufunga. Tulikuwa na fursa nyingi ambapo tulijiweka katika nafasi ambazo si nzuri na tukawa tunaleta krosi mbovu. Kwa hiyo nafikiri haikubaliki kucheza mchezo wa kushambulia kisha tusipate goli hata moja," alisema Drexler.

Katika wafungaji bora wa Bundesliga kufikia sasa Robert Lewandowski anaongoza akiwa na mabao 23 kisha mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt Andre Silva yuko kwenye nafasi ya pili na magoli 14 sawa na Erling Haaland, chipukizi wa Dortmund mwenye mabao 14 pia.

Fußball Bundesliga Schalke 04 v Bayern München | Tor 0:2 Lewandowski
Robert Lewandowski anaongoza jedwali la wafungaji boraPicha: Leon Kuegeler/Pool/REUTERS

Andrej Kramaric wa TSG Hoffenheim na Wout Weghorst wa VfL Wolfsburg wote wana mabao kumi na mbili na ndio wanaokamilisha orodha ya tano bora.