Bayern Munich yaanza vibaya sehemu ya pili ya msimu
31 Januari 2015Haikuwa siku njema kwa mabingwa hao wanaofundishwa na Kocha Pep Guardiola, ambao hadi wanakwenda mapumziko walikuwa hawajashindwa mechi yoyote msimu huu. Kwa muda wa dakika tisini tu, Wolfsburg ilikuwa imewabugiza magoli 4, idadi sawa na magoli iliyofungwa Bayern Munich katika mechi 17 za sehemu ya kwanza ya msimu huu.
Mnamo dakika ya tatu tu ya mchezo mholanzi Bas Dost aliunganisha pasi iliyochongwa na Daniel Caliguiri, na kuachia mkwaju ambao kipa Manuel Neuer wa Bayern Munich aliusindikiza kwa macho hadi kwenye kona ya wavu. Juhudi za Bayern kutaka kuzawazisha ziliishia pachungu, baada ya Wolfsburg kuwageuzia kibao, katika shambulizi lililohitimishwa kwa goli la pili lililotiwa kimiani na yule yule Bas Dost.
Mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu
Magoli mawili kwa nunge yaliwafanya wachezaji wa Bayern ambao hawakuzoea kujikuta katika hali hiyo wakipoteza subira, na kucheza rafu iliyopelekea kadi ya njano kwa kiungo wao Xabi Alonso, ambaye alionekana kupandwa na jazba. Hadi mapumziko ubao wa magoli ulionyesha Wolfsburg 2, Bayern Munich 0.
Kama mabingwa hao walidhani watarekebisha mambo katika kipindi cha pili ilikuwa ni ndoto tu, kwani ilikuwa Wolfsburg iliyoliona lango tena mnamo dakika ya 53 ya mchezo, kupitia mbelgiji Kevin de Bruyne, aliyekimbia nusu ya uwanja, na kumtumia salamu kipa Neuer kwa nduki kutoka umbali wa mita kumi.
Magoli matatu kwa sufuri ugenini yaliufanya mlima wa Bayern Munich kuwa mrefu, lakini kwenye dakika ya 55 Juan Bernat aliweza kurudisha bao moja ambalo liliishia kuwa pekee la kufutia machozi. Haikuishia hapo kwani kauli ya mwisho ilitoka kwa Wolfsburg mnamo dakika ya 73, pale yule yule Kevin de Bruyne aliposhindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Bayern Munich kwenye mechi hiyo kwa kupachika bao la nne.
Guardiola akubali kipigo
Akizungumza na waandishi wa habari baaya ya mechi, kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola hakuwa na ukaidi. ''Ni kweli walikuwa timu bora na walistahili ushindi'' alisema Guardiola, na kuongeza kuwa magoli yao yaliingia katika muda mbaya kwa Bayern, yaani dakika za mwanzoni na za mwishoni.
Kwa upande mwingine, kocha wa Wolfsburg Dieter Hecking amewapongeza vijana wake, akisema ushindi huu unawapa ari ya kuendelea kufanya vyema.
Kongo dhidi ya Kongo katika kombe la Afrika la Mataifa
Na katika michuano ya kombe la Afrika la Mataifa ambayo hii leo inaingia katika raundi ya robo fainali zitachezwa mechi mbili jioni ya leo, ya kwanza ikiwa kati ya watani wa jadi, Kongo Kinshasa na Kongo Brazzaville, ya pili itakuwa kati ya Tunisia, na wenyeji Guinea ya Ikweta.
Akizungumzia mechi dhidi ya watani wao wa Congo Brazzaville, kocha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Florent Ibenge, amesema ni mchezo kati ya ndugu wanaotenganishwa tu na mto Kongo. Kocha wa Kongo Brazzaville Claude Le Roy ambaye siku za nyuma aliifunza Kongo Kinshasa ameunga mkono kauli ya mpinzani wake, akisema utakuwa mchuano baina ya ndugu wanaojuana vyema, na kwamba hilo litaongeza msisimko.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape
Mhariri: Sudi Mnette