1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yafungua msimu bila mashabiki

18 Septemba 2020

Msimu mpya wa Ligi kuu ya kandanda Ujerumani - Bundesliga unaanza rasmi ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich wataanza kampeni ya kusaka taji lao la tisa mfululizo kwa kuwaalika Schalke katika dimba la Allianz Arena

https://p.dw.com/p/3ieUa
Sport I Training I FC Bayern I Leroy Sane
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Msimu mpya wa Ligi kuu ya kandanda Ujerumani - Bundesliga unaanza rasmi leo usiku ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich wataanza kampeni ya kusaka taji lao la tisa mfululizo kwa kuwaalika Schalke katika dimba la Allianz Arena. Hata hivyo, watafanya hivyo bila ya kiungo wao Mhispania Thiago Alcantara ambaye anajiunga na Liverpool.

Ina maana Bayern wamewapoteza wachezaji wanne kutoka kikosi chao kilichoshinda fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi uliopita. Ivan Perisic, Philippe Coutinho na Alvaro Odriozola wamerudi Inter Milan, Barcelona na Real Madrid mfululizo baada ya mikataba yao ya mkopo kukamilika.

Kulikuwa na habari mbaya zaidi baada ya mipango yao ya kuwaruhusu uwanjani mashabiki 7,500 kuzuiwa na meya wa Munich kwa sababu ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona. Hata hivyo, kiasi fulani cha mashabiki kwa mara ya kwanza tangu Machi wataruhusiwa kuingia viwanjani katika mechi nyingine za Bundesliga kuanzia kesho.