Bayern Munich yamnyakua Leroy Sane kutoka Man City
3 Julai 2020Mabingwa mara nane mfululizo wa ligi ya soka ya Ujerumani, Bundesliga, Bayern Munich, Ijumaa tarehe (03.07.2020) imethibitisha kunyakua saini ya winga wa Ujerumani Leroy Sane kutokea timu ya Manchester City kwa mkataba wa miaka mitano kwa dau lililoripotiwa kufikia angalau euro milioni 50.
"FC Bayern ni klabu kubwa sana na ina malengo makubwa, malengo haya yananifaa pia," alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye aliongeza kusema kuwa anataka kushinda ligi ya mabingwa barani Ulaya akiwa na vigogo hao wa Bundesliga.
"Natarajia changamoto mpya na siwezi kusubiri kufanya mazoezi na timu."
Sane anatazamia kuungana tena na kocha mkuu wa Bayern, Hansi Flick, ambaye ameiwezesha klabu hiyo kutwaa taji la nane mfululizo ikiwa ni msimu wake wa kwanza akishika mikoba ya kuwanoa vigogo hao wa soka nchini Ujerumani.
"Ninamfahamu Hansi Flick tangu timu ya taifa ya vijana walio chini ya umri wa miaka 21, tulikuwa na uhusiano mzuri sana huko," aliongeza Sane.
"Ninataka kushinda mataji mengi kadri iwezekanavyo na FC Bayern, na ligi ya mabingwa iko kileleni.
Mabingwa wa Bundesliga hawakutoa ada ya uhamisho lakini Sky Sports na BBC wameripoti kwamba Bayern na City walikubaliana ada ya paundi milioni 54.8 sawa na euro milioni 59.97.
Gazeti la kila siku la Bild la Ujerumani limeripoti kuwa ada hiyo ni karibu euro milioni 50.
"Tuna furaha kwamba tunaweza kumkaribisha Leroy Sane," alisema mwenyekiti wa klabu ya Bayern, Karl-Heinz Rummenigge.
"Yeye ni mchezaji bora ambaye amethibitisha sifa zake kwa miaka iliyopita, haswa katika timu ya taifa.
"Lengo letu ni kukusanya wachezaji bora wa Ujerumani katika timu ya FC Bayern na kujitolea kwa Leroy kunathibitisha hilo."
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ataanza kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao huko Munich wiki ijayo, klabu hiyo ilisema ikimaanisha hatakuwepo katika mchezo wa fainali wa kombe la DFB Pokal siku ya Jumamosi tarehe (04.07.2020) wakati mabingwa hao watakapopepetana na Bayer Leverkusen huko mjini Berlin.
Mnamo mwaka jana, Sane alikuwa ameripotiwa kuwa na uhamisho wa euro milioni tatu kuelekea Bayern kabla ya kupata jeraha kubwa la goti mnamo mwezi Agosti mwaka jana ambalo lilimuweka nje ya uwanja hadi mwezi Februari mwaka huu.
Chanzo/AFP