Bayern na Dortmund kuumana
3 Mei 2013Afisa Mkuu Mtendaji wa Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke amekiri kuwa klabu yake haina uhusiano mzuri na Bayern Munich. Hii ni baada ya habari kuchipuka wiki iliyopita kwua nyota wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 20 Mario Götze ameamua kuusitisha mkataba wake na Borussia ili kujiunga na Bayern mwezi Julai kwa kiasi kinachoripotiwa kuwa euro milioni 37.
Watzke amesisitiza kuwa hakuna uhasama baina ya vilabu hivyo, lakini ujumbe wa Bayern haujaalikwa kama kawaida kwa chakula cha mchana na wenzao wa Dortmund, na utasalimiwa kwa kupeana mikono.
Mario Götze anaondoka Dortmund
Dortmud watakosa huduma za Mario Götze, ambaye ana jeraha la mguu alilopata wakati wa mechu dhidi ya Real Madrid wiki iliyopita, wakati kiungo wa Ujerumani Sven bender akiwa mkekani pia.
Kocha wa Bayern Jupp Heynckes amesema mchezo wa leo hauna umuhimu wowote ikizingatiwa kwua tayari wao ni mabingwa wa Ujerumani, na kwa hivyo hatakichagua kikosi dhabiti kitakachocheza katika uwanja wa Dortmund, Signal Iduna Park.
Nafasi tatu za kwanza katika Bundesliga ni kama tayari zimechukuliwa, huku Bayer Leverkusen ikitarajiwa kujikatia tikiti ya mwisho ya kucheza msimu ujao katika Champions League. Wakati Greuther Fuerth wakiwa tayari wametimuliwa kutoka Bundesliga, nambari mbili kutoka nyuma Hoffenheim wanahitaji ushindi dhidi ya Werder Bremen, ambao pia wako pointi mbili tu kutoka eneo la kushushwa daraja.
katika mechi nyingine, Augsburg inahitaji pointi tatu itakapocheza nyumbani kwa Freiburg kesho Jumapili wakati wenyeji wao wakilenga kujitahidi kusalia katika nafasi ya sita ili kucheza katika Europa League msimu ujao.
Mechi nyingine za leo ni VfB Stuttgart v Greuther Fuerth, Hannover 96 v Mainz 05, Nuremberg v Bayer Leverkusen, na Eintracht Frankfurt v Fortuna Duesseldorf. Kesho Jumapili, Hamburg watafunga kazi dhidi ya VfL Wolfsburg
Mourinho anaondoka Real Madrid?
Jose Mourinho ambaye bila shaka katika siku za karibuni amegonga sana vichwa vya habari, amesisitiza kuwa hajaamua kama atasalia katika klabu ya Real Madrid kwa msimu wa nne kama kocha. Mreno huyo alisema Jumanne iliyopita baada ya timu yake kubanduliwa nje ya nusu fainali ya Champions League kuwa huenda asirudi tena Real Madrid msimu ujao. Alidokeza kuwa huenda akarudi England, ambako anahusishwa na kazi ya kuifunza klabu yake ya zamani Chelsea.
Lakini jana Ijumaa, Mourinho alikuwa na maneno ya ukarimu kwa Chelsea, mahali ambako anasema alipendwa sana, kinyume na jinsi ilivyo Uhispania. Alisema yeye huondoka vilabu anavyosimamia kwa roho safi kama tu ilivyokuwa katika Chelsea. Mreno huyo ambaye mkataba wake na Real Madrid unakamilika mwishoni mwa mwaka wa 2016, amesisitiza kuwa atasubiri hadi mwishoni mwa msimu huu ili kufanya mazungumzo na rais wa Madrid Florentino Perez kuamua kama wakati umewadia wa kuwachana. Jose Mournho kwa jina la utani The Special One anapendwa sana na mashabiki wa klabu ya Chelsea ambao wamekuwa wakimpigia upatu Mreno huyo kurudi katika uwanja wa Stamford Bridge.
Madrid watawaalika watani wao Atletico Madrid mnamo Mei 17 katika fainali ya Copa del Rey. Madrid inatarajiwa kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Barcelona.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman