1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern sasa jukumu lake ni kuifukuza BVB

Sekione Kitojo
17 Desemba 2018

Bayern Munich  yaifukuzia  Borussia  Dortmund  kabla  ya  kumalizika kipindi  cha  kwanza  cha  ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga.

https://p.dw.com/p/3AGpZ
Fußball Bundesliga Hannover 96 - Bayern München | Jubel
Wachezaji wa Bayern Munich wakikumbatiana kwa furaha wakishangiria baoPicha: picture-alliance/dpa/M. Sohn

Tukihamia  katika  ligi  sasa , tuanze  na  Bundesliga: Bayern Munich imeanza kucheza  kandanda linaloleta  tija  katika  jukumu  lake  jipya ambapo  hivi  sasa jukumu  lake  ni  kuifukuza  Borussia  Dortmund viongozi wa  Bundesliga  kwa  sasa  lakini   timu  hiyo  kutoka  jimboni Bavaria  imeanza  kurejea  tena  katika  ushindi  wakati  ikiingia  katika mtihani  wake mkubwa  dhidi  ya  RB Leipzig hapo  Jumatano.

Bayern  inapishana  na  Dortmund  kwa  pointi 9  wakati  ikiingia  katika mchezo  wa  katikati  ya  wiki  na  mwanya  huo  unaweza  kuongezeka hadi  pointi  12 , hata  kama itakuwa  ni  kwa  muda , iwapo Dortmund inayosafiri  kwenda  mjini  Dusseldorf  kupambana  na  Fortuna Dusseldorf kesho  Jumanne.

Dortmund  imeshinda  michezo 6 ya  Bundesliga  mfululizo  na  kujenga mwanya  huo  dhidi  ya  Bayern  Munich  inayoshikilia  nafasi  ya  tatu pamoja  na Borussia  Moenchengladbach , ambao  wako  katika  nafasi  ya pili kutokana  na  tofauti  ya  mabao ya  kufunga.

Lakini baada  ya  kipindi  cha  kuyumba , Bayern  wameanza  kupata  tena mbinu  za  ushindi  kwa  kushinda  mata  tatu  mfululizo  katika  ligi  na kufikia  kilele  chake  mwishoni  mwa  juma  kwa  ushindi  wa  mabao 4-0 dhidi  ya  Hannover 96, ushindi  ambao  kocha  Niko Kovac ameuita ushindi  huo  kama „moja  ya mchezo  wao  mzuri  kabisa  msimu  huu."

Leipzig , ambayo  iko  pointi 2 tu  nyuma  ya  Bayern ikiwa  katika  nafasi ya  nne, itatoa  changamoto  kubwa  kuliko  ilivyokuwa  kwa  kikosi  cha Hannover 96  kilichoko  mkiani  katika  msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani Bundesliga, lakini  hali  ya  kujiamini  imeanza  kurejea  katika  kikosi  cha Bayern.

Bundesliga: Leipzig-Mainz
Wachezaji wa RB Leipzig wakishangiria bao dhidi ya FSV MainzPicha: Getty Images/AFP/R. Michael

Gladbach kupunguza mwanya

Gladbach inaweza  kupunguza  mwanya dhidi  ya  Dortmund  hadi pointi sita, iwapo  hata  kama  ni  kwa  muda  tu, kwa  pambano  la  mapema kesho  Jumanne , ambapo  inapambana  na  Nuremberg nyumbani. Kocha Dieter Hecking  alikiri  kwamba  kikosi  chake  cha  Gladbach  kilikuwa  na bahati  tu  kupata  pointi  moja  katika  mchezo  dhidi  ya  Hoffenheim  siku ya  Jumamosi, ambapo  timu  hizo  zilitoka  sare  bila  kufungana, na  pia kuwapoteza wachezaji  muhimu  kama  Raffael  na Lars Stindl ambaye huenda  asiwemo  katika  kikosi kitakachopambana  na Nuremberg.

Fußball Bundesliga TSG 1899 Hoffenheim vs Borussia Mönchengladbach
Andrej Kramaric (kushoto ) akipambana na Michael Lang wa Gladbach(kulia)Picha: Getty Images/AFP/D. Roland

Dortmund  hivi  karibuni  iliwadhibiti  mahasimu  wao  wakubwa  Schalke 04  na  pia  kuwatupa  kando  Werder  Bremen  ambayo  inawania kushiriki  katika  vikombe  vya  Ulaya  msimu  ujao na  kufanikiwa  kupata taji  ambalo  si  rasmi  la  „mabingwa  wa  mapukutiko" kabla  ya  michezo miwili  ya kukamilisha  mzunguko  wa  kwanza  wa  Bundesliga.

Lakini kwa  ubingwa wake  wa  kwanza  tangu  mwaka  2012, kukiwa  na uwezekano  wa  hilo,  kikosi  hicho  cha  kocha  Lucien Favre  kina  shauku kutoteleza  dhidi  ya  Dusseldorf  ambayo  inapambana  kutoshuka  daraja , kabla  ya  kuukamilisha  mwaka  2018  kwa  pambano  kali  nyumbani dhidi  ya  Gladbach siku  ya  Ijumaa.

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Werder Bremen
Jadon Sancho (kulia) Paco Alcacer na Marco Reus wakikumbatiana baada ya BVB kupata baoPicha: Reuters/L. Kügeler

Bado tuna  michezo  miwili  muhimu kabla  ya  kwenda  katika  mapumziko ya  majira  ya  baridi na  tunataka  kuendelea  na  ushindi  hali tuliyoionesha  hadi  sasa  hadi  mwisho wa  nusu  ya  kwnza  ya  msimu ," amesema  mlinda  mlango  Roman Burki.

Tunafurahia hali  hii, lakini tunafahamu  pia  kwamba  hali  inaweza  kubadilika haraka.tunapaswa kufanya  kila  liwezekanalo katika  uwezo  wetu  kubakia  juu." Mapambano  ya  kesho  Jumanne  ni  pamoja  na  Hertha  Berlin ikiikaribisha  Augsburg  na  Wolfsburg  inaikaribisha  VFB Stuttgart, ambayo huenda  haitakuwa  na  nahodha  wake  Christian Gentner kutokana  na kuomboleza  kifo  cha  baba  yake  aliyefariki  siku  ya  Jumamosi baada  ya ushindi  wa  Stuttgart  dhidi  ya  Hertha Berlin.

Mwandishi: Sekione  Kitojo  / rtre / afpe / ape

Mhariri:  Iddi Ssessanga