Bayern yaelekea kutwaa ubingwa wa saba Bundesliga
6 Mei 2019Bayern Munich imejisogeza karibu na ubingwa wake wa saba mfululizo katika Bundesliga wakati imebaki michezo miwili baada ya kufungua mwanya wa pointi nne dhidi ya Borussia Dortmund kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Hanover 96. Borussia Dortmund iliteleza pale ilipolazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Werder Bremen siku ya Jumamosi.
Frank Ribery ataondoka Bayern Munich mwishoni mwa msimu lakini mwishoni mwa juma lijalo anaweza kuwa mchezaji pekee katika Bundesliga katika historia akiwa na mataji tisa katika jina lake.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye alijiunga na Bayern mwaka 2007, ameshinda mataji makubwa 21 akiwa na Bayern. Kwa ushindi dhidi ya RB Leipzig Jumamosi ijayo anaweza kuondoka akiwa na mataji tisa.
Pizzaro mchezaji mkongwe
Mchezaji wa Werder Bremen Claudio Pizzaro alipachika bao dhidi ya Borussia Dortmund baada ya kuingia uwanjani akiwa mchezaji wa akiba. Ni bao la 20 la mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 40 akiwa mchezaji wa akiba, likimuweka nyuma tu ya mfungaji bora wa muda wote Nils Petersen wa Freiburg.
Bayer Leverkusen wameshinda michezo minne mfululizo, kiwa ni pamoja na mchezo wao wa jana Jumapili ambapo waliirarua Eintracht Frankfurt ambao ni timu inayowania pia kucheza katika Champions League msimu ujao kwa mabao 6-1, na kuwa sawa kwa pointi katika nafasi ya tano ya ligi wakipambana kuwania kungia katika timu nne bora za Bundesliga.
Ni mara ya kwanza kwa Leverkusen kupachika mabao 6 katika nusu ya kwanza ya mchezo katika ligi.
Katika Bundesliga wakati huu ikiwa imesalia michezo miwili ligi kumalizika, kuna mpambano wa kuwania kuingia katika timu nne bora ambazo zitakuwa na fursa ya kucheza katika Champions League msimu ujao na pia kuna vuta nikuvute wa kuwania ubingwa.
Bayern Munich imefungua mwanya wa pointi nne dhidi ya Dortmund lakini kinyang'anyiro hicho hakijamalizika kwani Borussia Dortmund inasema lolote linaweza kutokea na Bayern ikateleza kama ilivyoteleza yenyewe mwishoni mwa juma hili kule Bremen..
Schalke yasuasua
Schalke 04 imefanya vya kutosha kupata sare ya bila kufungana dhidi ya Augsburg kujihakikishia kubakia katika ligi daraja la kwanza Bundesliga licha ya msimu uliojaa matatizo. Lakini ni mara ya nane wanashindwa kupata bao katika mchezo wa nyumbani msimu huu, ikiwa ni mara nyingi zaidi ya misimu mingine ya Bundesliga. Wameshindwa pia kushinda katika michezo saba ya nyumbani , ikiwa ni rekodi yao mbaya kabisa tangu mwaka 1992.