Bayern yainyoosha BVB
8 Aprili 2019Ule mchezo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa kati ya Bayern Munich na Borussia Dortmund hatimaye ulifanyika siku ya Jumamosi, lakini pambano hilo linalofahamika kama Klassiker hapa Ujerumani halikukidhi matarajio ya wengi, pale Borussia Dortmund iliposhindwa kabisa kuhimili vishindo vya kaka mkubwa Bayern Munich na kubugia mabao 5-0.
Mchezo huo ulikuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa kutokana na kwamba mchezo wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund uliishia kwa ushindi wa Dortmund wa mabao 3-2 dhidi ya Bayern Munich. Pili ni kwamba Borussia Dortmund ilipoingia katika mchezo huo wa jumamosi ilikuwa ikiongoza jedwali la msimamo wa ligi kwa pointi mbili, mbele ya bayern Munich.
Kwa hivyo kila mpenda kandanda alitarajia kwamba mara hii ubingwa wa Ujerumani utaamuliwa kwa timu hizo kuvutana. Lakini yaliyotokea yanafurahisha:Bayern Munich iliirarua bila huruma Borussia Dortmund kwa mabao 5-0 na kuwaburuza Dortmund muda wote jioni hiyo.
Bayern Munich kwa ushindi huo unaongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja , ikiwa na pointi 64 na Borussia Dortmund ikiwa na pointi 63. RB Leipzig imejiimarisha katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 55, wakati Eintracht Frankfurt inakumbukia enzi zake za kina JJ Okocha na Antony Yeboah wakati nayo ikijiimarisha katika nafasi ya nne ya kucheza katika Champions League msimu ujao ikiwa na pointi 52. Frankfurt iliishinda Schalke 04 siku ya Jumamosi kwa mabao 2-1, nyumbani kwa Schalke.
Wakati huo huo upangaji wa timu zitakazopambana katika nusu fainali ya kombe la shirikisho nchini Ujerumani , DFB Pokal ni kwamba Bayern Munich itakwaana na Werder Bremen , na Hamburg SV itaikaribisha RB Leipzig kuamua nani anakwenda Berlin katika fainali ya kinyang'anyiro hicho.