Bayern yajipanga kwa michuano ya kabla ya kuanza msimu
22 Mei 2015Kikosi hicho cha Pep Guardiola , ambacho kimeondolewa katika nusu fainali ya Champions League na Barcelona wiki iliyopita , kitafungua ziara yao kwa pambano dhidi ya Valencia katika uwanja wa kiota cha ndege mjini Beijing Julai 18 kabla ya kwenda Shanghai kupambana na Inter Milan siku tatu baadaye.
Watakamilisha ziara yao kwa mchezo dhidi ya mabingwa wa Champions League ya bara la Asia mwaka 2013 Guangzhou Evergrande, timu ambayo imeshinda ligi ya Uchina mara nne mfululizo.
Bayern , timu tajiri kabisa nchini Ujerumani ikiwa na mapato yanayofikia nusu bilioni katika msimu uliopita inatafuta soko kubwa kabisa la Asia ili kuendeleza ukuaji wake wa mapato na mara ya mwisho kuitembelea China ilikuwa mwaka 2012.
Kwingineko, Osaka na Yokohama itakuwa miji itakayokuwa mwenyeji wa michezo ya kombe la dunia la vilabu mwaka 2015 nchini Japan, shirikisho la kandandfa duniani FIFA limesema jana Ijumaa. Yokohama utakuwa mji ambapo fainali itafanyika katika mashindano hayo yatakayoanza Desemba 10-20 zikikutanisha mabingwa wa mashirika ya mabara sita wanachama wa FIFA na timu kutoka nchi wenyeji, ambapo itakuwa ni mshindi wa ligi ya Japan mwaka 2015.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef