Bayern yakwaa kisiki
29 Oktoba 2012Maamuzi yasiyoridhisha pia yalitokea katika mpambano wa watani wa jadi Everton na Liverpool na Bayern Munich yaonja chungu ya kupigwa mwereka katika bundesliga, wakati mabingwa Borussia Dortmund na Schalke 04 baada ya ushindi mnono katika Champions League , zang'ara.
FC Bayern imekwaa kisiki wiki hii, pale mfululizo wake wa ushindi katika michezo minane ya Bundesliga ulipopigwa full stop na Bayer Leverkusen katika mchezo uliofanyika jana jioni. Bayern iliangukia pua baada ya kukubali kipigo cha mabo 2-1, na kuvutwa shati katika mbio zake katika uongozi wa ligi hiyo.
Hata hivyo Bayern inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na points 24 ikifuatiwa na Schalke 04 ambayo ina points 20. Mabao ya Stefan Kiessling na bao la kujifunga wenyewe la Jerome Boateng yalihakikisha ushindi wa kwanza wa Leverkusen tangu miaka 23 uwanjani Allianz Arena dhidi ya Bayern.
Michezo mingine jana ilizikutanisha Hannover 96 na Borussia Moenchengladbach. Hannover ilipoteza ushindi wa mabao 2-0 na kupigwa mwereka wa mabao 3-2 mwishoni katika mpambano huo, ambao ulikuwa wa vuta nikuvute.
Frankfurt nayo yagonga ukuta
Hapo kabla VFB Stuttgart iliizamisha Eintracht Frankfurt , ambayo imeanza msimu huu kwa kushangaza mashabiki wa soka kwa kushinda michezo yake sita ya mwanzo. Stuttgart hata hivyo haikuwa na kazi nyepesi kupata ushindi huo , lakini mabao 2-1 yalitosha kwa kikosi hicho cha kocha Bruno Labadia kurejea nyumbani na points tatu muhimu .
Borussia Dortmund ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Freiburg katika mchezo ambao uamuzi pia ulilalamikiwa mno na Freiburg, kwamba mabao yote ya Dortmund hayakupaswa kukubaliwa, na Freiburg kunyimwa penalti, baada ya Leverndowski kuunawa mpira katika harakati za kuokoa langoni mwake.
VFL Wolfsburg ambayo imejitenga na kocha wake aliyeitawaza bingwa miaka minne iliyopita Felix Magath, wiki iliyopita , imefanya maajabu kwa ushindi wa mabao 4-1 nyumbani kwa Fortuna Dusseldorf siku ya Jumamosi na kuchupa kutoka mkiani mwa ligi na kushika nafasi ya tatu kwa kuwa na points nane.
Huko Uingereza jana Jumapili(28.10.2012) soka ya nchi hiyo iliingiwa na mdudu tena kutokana na madai ya ubaguzi na timu kubebwa na waamuzi. FC Chelsea imetoa madai rasmi kuhusiana na lugha, ambayo inaripotiwa kuwa , refa wa mchezo huo dhidi ya Manchester United aliitoa dhidi ya wachezaji wawili wa Chelsea jana, katika matokeo yenye utata , ambapo Chelsea ilicheezea kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Man United.
Kabla ya hapo mashabiki wa soka walishuhudia bao la ushindi la Liverpool likikataliwa na mwamuzi akidai mfungaji wa bao hilo Suarez alikuwa ameotea. Lakini bao la ushindi la Manchester United lilikubaliwa hata kama mfungaji wa bao hilo Chicharito alionekana kutokea katika nafasi ambayo alikuwa ameotea.
Moyes ataka kadi nyekundu
Wakati huo huo kocha wa Everton David Moyes anahisi kuwa Luis Suarez wa Liverpool alipaswa kutolewa nje kwa kadi nyekundu hata kabla ya juhudi za mwisho za mshambuliaji huyo wa Liverpool kupata bao la ushindi dakika za mwisho za mchezo huo kukataliwa na mwamuzi katika mchezo wao wa watani wa jadi wa Merseyside.
Kwa mara nyingine tena raia huyo wa Uruguay alikuwa kivutio katika uwanja wa Goodison Park, baada ya kupachika bao la kwanza ambalo liliingizwa wavuni na mchezaji wa Everton , Leighton Baines mapema katika mchezo huo na kisha Luis Suarez kushangiria kwa kujitupa chini miguuni mwa kocha wa Everton , Moyes.
Kabla ya mchezo huo , kocha wa Everton alikuwa na mawazo kuwa Suarez hujiangusha kirahisi langoni mwa adui na kwamba kitendo kama hicho husababisha mashabiki kutokuja uwanjani kushuhudia pambano.
Cristiano atamba
Katika La Liga nchini Uhispania Gonzalo Higuain na Cristiano Ronaldo walipachika kila mmoja mabao 2 wakati wa ushindi wa Real wa mabao 5-0 dhidi ya Mallorca jana na kuendelea kuweka mbinyo katika timu zinazoongoza ligi hiyo.
Wakati huo huo Atletico Madrid iliishinda Osasuna kwa mabao 3-1 na kuendelea kuwa sawa na Barcelona kwa points.
Viongozi wa Serie A Juventus Turin imeendelea kupeta kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Catania baada ya timu hiyo kutoka kisiwa cha Sicily kupata bao ambalo lilionekana kuwa halali lakini mwamuzi alilikataa.
Bao la Juve hata hivyo lilionekana kuwa si halali kwa kuwa mshambuliaji Nicklas Bendtner alikuwa ameotea wakati alipopiga mpira ambao uliokolewa na mlinda mlango wa Catania na kusababisha Arturo Vidal kuukwamisha mpira huo wavuni.
Na huko nchini Argentina, lile pambano la watani wa jadi ambalo linazungumziwa kuwa huwa la aina ya pekee duniani kwa ushindani , lilimalizika kwa sare ya mabo 2-2 kati ya Boca Juniors na River Plate.
Tennis.
Victoria Azarenka kutoka Belarus hajashinda ubingwa wa chama cha Tennis duniani , WTA , lakini kufikia nusu fainali kumemhakikishia kushika nafasi ya kwanza katika orodha ya wachezaji bora wa tennis kwa upande wa wanawake msimu huu.
Azarenka anafuatiwa na Maria Sharapova wa Urusi pamoja na Serena Williams wa Marekani akishika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa wanaume mchezaji anayeongoza orodha hiyo ni Roger Federer wa Uswisi, akifuatiwa na Novak Djokovic wa Serbia na Andy Murray wa Uingereza anashikilia nafasi ya tatu.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre / zr
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman