Bayern yanyakua ubingwa wa mataji mawili ya msimu
27 Mei 2019Sherehe rasmi za ubingwa wa Bundesliga pamoja na kunyakua ubingwa wa kombe la shirikisho kwa Bayern Munich hapo jana mjini Munich. Mashabiki wa Bayern Munich walisherehekea ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya RB Leipzig jana, ushindi ambao umewapatia mabingwa hao kombe hilo la DFB Pokal kwa mara ya 19 na kuwezesha kukamilisha ushindi mara mbili wa ligi pamoja na kombe kwa pamoja katika msimu mmoja. Maelfu ya mashabiki wa bayern waliujaza uwanja wa Marienplatz mjini Munich kwa kuimba nyimbo na kucheza katika sherehe hiyo pamoja na kikosi cha Bayern Munich kilichofanikisha hatua hiyo wakijitokeza pamoja na mataji hayo mawili.
Ni mara ya 12 kwa bayern kupata ushindi wa mataji mawili katika msimu mmoja wakati kocha Niko Kovac , ambaye alinyakua ubingwa wa kombe hilo akiwa na Eintracht Frankfurt msimu uliopita na kuiongoza timu hiyo kuingia fainali katika mwaka 2017, amekuwa mtu wa kwanza kushinda mataji mawili na Bayern akiwa mchezaji na pia kama kocha.
Akiwa katika baraza ya juu ya jengo ilipofanyika sherehe hiyo kocha Niko Kovac aliwashukuru wafuasi wa Bayern kwa kusema:
"Hatimaye lakini sio mwisho, napenda niwashukuru nyie wote. Nyie , ambao wiki baada ya wiki mmetufuata ikiwa nyumbani ama nje ya hapa. Tumekuwa na nyakati ngumu lakini, lakini mmetuunga mkono, katika nyakati mbaya na nzuri. Mlikuwa kila wakati nasi. Hatungeweza kufanikiwa bila nyie, na jana pia tusingefanikiwa. Ndio sababu nasema tunawashukuru sana. Bakini kama mlivyo. Nawapenda na nawatakia kila la kheri."
Mashabiki pia walipata fursa ya kuwaaga Frank Ribery ambaye amecheza kwa mara ya mwisho dhidi ya RB Leipzig akiwa na klabu hiyo, na Arjen Robben , ambao wote wanaondoka kutoka katika kikosi hicho. Ribery alisema.
"Tumeshinda pamoja na mnafahamu, itabaki kuwa hivyo milele, hatuwezi kusahau kile tulichokifanya kwa pamoja. Ahsante kwa kila kitu, asante kwa timu yangu. Nawapenda. Asanteni sana."
Nae Arjen Robben, akiwaaga mashabiki wa FC Bayern alisema:
"Ningependa tu kuwashukuru. Ilikuwa miaka 10 ya mafanikio. Tumesherehekea mataji mengi pamoja. Tulipata mafanikio makubwa. familia yangu na mimi tumejisikia tuko nyumbani hapa tangu siku ya mwanzo na kwa hiyo nawashukuru na nitaendelea kuwa mmoja wetu."
Wakati huo huo rais wa Bayern Munich Uli Hoeness ameonesha kumuunga mkono kocha Niko Kovac na kumshauri mlinzi wa kati wa Bayern Munich Jerome Boateng kutafuta klabu nyingine wakati wa sherehe za ubingwa wa ligi na kombe la shirikisho mjini Munich jana Jumapili. Ushindi huo umeondoa tetesi kuhusiana na Kovac, kwamba huenda kibarua kikaota majani baada ya kufanya vibaya mwanzoni mwa msimu huu.
Akiulizwa iwapo Kovac , ambaye ana miaka mingine miwili zaidi katika mkataba wake baada ya msimu wake wa kwanza akiwa Bayern, atakuwa kocha msimu ujao, Hoeness alijibu ; " kwa asilimia 100, ndio."
Lakini Hoeness ameweka wazi kwamba klabu hiyo inatarajia mengi kimataifa baada ya Bayern kutupwa nje ya Champions League dhidi ya Liverpool katika mchezo wa timu 16 zilizobakia katika Champions League.
Hoennes hata hivyo amesema Boateng mwenye umri wa miaka 30 , ambaye hakutumika siku ya Jumamosi katika mchezo wa kombe la Ujerumani na sio tena chaguo la kwanza chini ya kocha Nico Kovac , anapaswa kutafakari kuondoka klabuni hapo licha ya kuwa na mkataba hadi mwaka 2021.
Bayern Munich kwa hiyo itakutana na Borussia Dortmund katika kombe la Super Cup msimu ujao hapo Agosti 3 , limesema shirikisho linaloendesha ligi ya Ujerumani DFL leo Jumatatu.