Bayern yapata kipigo cha pili msimu huu dhidi ya Leipzig
19 Machi 2018Borussia Dortmund ilijiimarisha katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga baada ya kupata ushindi mwembamba lakini muhimu dhidi ya Hannover 96 na kufikisha pointi 48, baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 jana Jumapili.
Baada ya kutolewa na RB Salsburg ya Austria katika mashindano ya Europa League katikati mwa juma lililopita , Borussia Dortmund ilionekana kuwa na nia ya kutaka ushindi tangu mwanzo wa mchezo na ilifanya hivyo baada ya mshambuliaji wake Michy Batshuayi kuuweka mpira wavuni, ikiwa hilo ni bao lake la 6 katika michezo 7 ya Bundesliga tangu ajiunge na kikosi hicho kutoka Chelsea ya mjini London kwa mkopo.
Huyu hapa nahodha wa Borussia Dortmund Marcel Schmelzer:
"Nafikiri, tumeona, kwamba tumeonesha tunataka kushinda na hilo tumelionesha katika kipindi cha kwanza bila shaka. Katika kipindi cha pili kila mmoja wetu alipungukiwa na nguvu na ndio sababu tunafurahi, kwamba kwa sasa tutapumzika kwa wiki mbili."
Bayern Munich ilipoteza mchezo wake wa pili msimu huu chini ya kocha Jupp Heynckes jana Jumapili dhidi ya RB Leipzig, licha ya kwamba kipigo hicho hakitaathiri mwendo wa timu hiyo kuelekea ubingwa wake mara ya 6 mfululizo. Kocha Jupp Heynckes hajashitushwa sana na kipigo hicho lakini mlinzi Mats Hummels alionya kwamba timu hiyo inapaswa kucheza vizuri zaidi katika michuano inayokuja ya Champions League katika duru ya robo fainali.
Bayern Munich inapambana na sevilla ya Uhispania katika mchezo wa robo fainali ya Champions League. Bayern inauwezo wa kupandisha kiwango chake inapohitajika lakini kipigo cha jana Jumapili bila shaka kitachelewesha sherehe zake za kutawazwa mabingwa katika Bundesliga.
Bayern yapata kipigo
Bayern itaikaribisha Borussia Dortmund katika mchezo ujao Machi 31, lakini itatawazwa mabingwa mara ya 6 mfululizo iwapo Schalke 04 inayoshika nafasi ya pili haitaweza kuishinda Freiburg siku hiyo.
Kipigo hicho cha kwanza mwaka huu cha mabao 2-1 dhidi ya RB Leipzig kimeipandisha timu hiyo ya mjini Leipzig hadi katika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 43. Mshambuliaji wa RB Leipzig Timo Werner anazungumzia utamu wa ushindi dhidi ya Bayern.
"Wakati ukifunga bao dhidi ya Bayern inafurahisha sana. Na iwapo mnashinda dhidi ya bayern inapendeza zaidi. Leo tumecheza vizuri sana. Tulikuwa tunacheza kwa nguvu, na hatukuwaruhusu Bayern kuandaa mchezo wao. Na hii ni lazima kusema. Tulikuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Bayern na tulibadilisha matokeo hayo, katika mtindo , ambao timu bora kabisa inavyofanya. Kwa hilo tunastahili kujisikia fahari."
Eintracht Frankfurt inapiga hatua kuelekea kucheza katika Champions League ama katika Europa League, na kila mchezo inaonesha ukomavu na mbinu za hali ya juu kuweza kubakia katika nafasi hiyo. Frankfurt chini ya kocha Nico Kovac imeimarika katika nafasi zote na iliibwaga Mainz 05 kwa mabao 3-0 siku ya Jumamosi na kujiimarisha katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 45.
Timu ya Hamburg SV ambayo haijawahi kushuka daraja tangu pale Bundesliga ilipoanzishwa mwaka 1963 imeonekana msimu huu kuparaganyika kabisa, na sio uwanjani tu hata nje ya uwanja.
Hamburg yasambaratika
Mlinzi Papadopolus baada ya kulalamikia uongozi wa timu hiyo ameweka nje ya uwanja na pia mchezaji wa kati Mbrazil Walace nae aliondolewa kutoka katika kikosi hicho kutokana na utovu wa nidhamu.
Matokeo ya mchezo wa 27 wa Bundesliga hayakuwa mazuri pia kwa timu hiyo pale ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Hertha Berlin na hatimaye kuchungulia mlango wa kuelekea daraja la pili ambapo timu hiyo imebakia na pointi 18 , na ikiwa ya mwisho kabisa.
Hali hiyo imekuja baada ya majirani zao katika msimamo wa ligi FC Kolon kupata ushindi wa kishindo wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa jadi Bayer Leverkusen jana mjini Kolon.
FC Koln imefikisha sasa pointi 20 mbili juu ya Hamburg ikiwa katika nafasi ya 17 na ikijaribu kuivuta chini Mainz 05 yenye pointi 25. Kolon imefufua matumaini yake ya kubakia katika daraja la kwanza kwa kucheza mchezo safi wenye ushindani dhidi ya Bayer Leverkusen na kutoka uwanjani kifua mbele katika mchezo huo wa watani wa jadi.
Huyu hapa mlinda mlango wa FC Kolon Timo Horn.
"Bila shaka hii inatufanya tujisikie vizuri. Tunajitahidi kwa kweli kufanya kila kitu. Nafarijika kuona kwamba tumeshinda michezo miwili ya Derby hapa nyumbani. Hakuna mtu anaweza tena kuondoa hilo, hata kama mwishoni itakuwaje."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef