Bayern yaporwa ushindi na Freiburg
5 Novemba 2018Kwa shuti moja tu kuelekea golini SC Freiburg ilifanikiwa siku ya Jumamosi kuikaba koo Bayern Munich na kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika uwanja wa Alianz Arena mjini Munich, ikiwa ni mara nyingine tena kikosi hicho cha kocha Nico Kovac kuonesha mchezo dhaifu, na kuendeleza mjadala juu ya uwezo wa kocha huyo katika kikosi cha Bayern.
Matokeo hayo yanaiweka Bayern Munich mabingwa watetezi wa Bundesliga msimu kuwa nyuma ya Borussia Dortmund kwa pointi nne. Borussia Dortmund ilifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 mbele ya VFL Wolfsburg, ikijipasha joto kwa pambano lao mwishoni mwa juma.
Borussia Dortmund inakaribisha Bayern Munich siku ya Jumamosi katika pambano la el Classico nchini Ujerumani.
Bayer 04 Leverkusen ililazimishwa kupiga magoti mbele ya Hoffenheim baada ya kucharazwa kwa mabao 4-1 nyumbani, kipigo ambacho kimesimamisha matumaini ya ushindi mfululizo wa Leverkusen katika Bundesliga baada ya kuitwanga Werder Bremen mabao 6-2 katika mchezo wa wiki ya 9 ya Bundesliga na pia ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach katika kombe la shirikisho DFB Pokal .
Katika msimamo wa ligi kuna mvutano mkubwa kuelekea kuwania nafasi nne za juu ili kucheza katika Champions League msimu ujao, pamoja na Europa league.
Borussia Dortmund iko kileleni ikiwa na pointi 24 , wakati Borussia Moenchenglandbach iko katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 20 , sawa na Bayern Munich iliyoko katika nafasi ya tatu, na inafuatiwa na RB Leipzig yenye pointi 19, timu hizo tatu zikipishana tu kwa pointi moja.
Eintracht Frankfurt iko katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 17 sawa na Werder Bremen , na TSG Hoffenheim iko katika nafasi ya 7 ikiwa na pointi 16 sawa na Hertha Berlin.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / dpae / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman