Bayern yarejea kileleni mwa Bundesliga
21 Oktoba 2013Katika mpambano wa kuvutia jana Jumapili kati ya Hamburg SV na VFB Suttgart, vigogo hivyo vya soka la Ujerumani vilitoshana sare ya mabao 3-3. Na katika mchezo wa mwisho jana jioni uliofikisha mwisho mchezo wa 9 wa Bundesliga , Wolfsburg ilishinda baada ya kuonesha mchezo dhaifu katika kipindi cha kwanza dhidi ya Augsburg na kujipatia points tatu za kwanza ugenini. VFL Wolfsburg ilipata ushindi wa mabo 2-1.
Mabingwa watetezi wa Bundesliga Bayern Munich walirejea kileleni mwa ligi hiyo wakiipora nafasi hiyo kutoka kwa Leverkusen. Kikosi cha Leverkusen kilfadika na bao hewa la Kießling siku ya Ijumaa dhidi ya Hoffenheim. BVB , Borussia ilipata ushindi wa taabu wa bao 1-0 dhidi ya Hannover kama ilivyokuwa kwa Schalke 04 ambao walikuwa wageni wa wageni katika ligi hiyo Braunschweig ambao Schalke ilipata ushindi wa kubana wa mabao 3-2.
Nürnberg na Freiburg zilitoshana sare ya bao 1-1, lakini bado zimeshindwa kupata ushindi. Siku ya Jumamosi Hertha BSC Berlin iliishinda Gladbach kwa bao 1-0 na kuchupa hadi nafasi ya nne.
Kwingineko katika bara la Ulaya ,
Mabingwa wa La Liga ligi ya Uhispania Barcelona walishindwa kuuona wavu siku ya Jumamosi kwa mara ya kwanza katika michezo 65 iliyocheza baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Osasuna.
Atletico Madrid ikakubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Espanyol wakati Real Madrid iliibuka kidedea kwa kupata ushindi wa tisa mfululizo.
Fiorentina iliirarua Juventus Turin kwa mabao 4-2 baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0, na kuipa Juventus kipigo chake cha kwanza msimu huu katika Serie A nchini Italia.
AS Roma nayo ikainyoa bila maji SSC Napoli kwa mabao 2-0.
Nchini Uingereza Arsenal London imeongeza uzito katika kampeni yake ya kuwania ubingwa msimu huu baada ya kuweka wavuni mabao 4 dhidi ya Norwich City wakati mchezaji wa kati Mesut Ozil akionesha uwezo mkubwa wa kuiunganisha timu hiyo. Arsenal iko points mbili juu ya msimamo wa ligi ikifuatiwa na Chelsea.
Manchester City na Tottenham Hotspurs zilipata ushindi mwishoni mwa juma, lakini hali ya wasi wasi inawakumba mabingwa watetezi Manchester United baada ya kushindwa kupata kama kawaida yao ushindi wa kufuatana na kuiacha timu hiyo ikiwa katika nafasi ya nane.
Champions League
Kinyang'anyoro cha Champions League kinarejea uwanjani kesho Jumanne na Jumatano. Arsenal London na Barcelona ni timu mbili ambazo zinawania kupata ushindi wa tatu katika michezo mitatu ya makundi yao.
Viongozi hao wa Premier League Arsenal na Borussia Dortmund makamu bingwa wa Champions League walikabiliana katika msimu wa mwaka 2011-2012 wakati Robin van Persie alipofanikisha ushindi wa Arsenal nyumbani. Mchezo wa pili ulikuwa sare ya bao 1-1 mjini Dortmund.
Schalke 04 pia itakuwa uwanjani kesho Jumanne ikioneshana kazi na Chelsea London . Chelsea inahitaji kwa udi na uvumba ushindi mjini Gelsenkirchen kupata kujiamini zaidi baada ya ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Steaua Bucharest katika kundi E. Michezo mingine ni kati ya Steaua Bucharest ikiikaribisha Basel ya Uswisi, Marseille ya Ufaransa inakuwa mwenyeji wa SSC Napoli ya Italia, wakati katika kundi G , Porto ya Ureno imewaalika Zenit St Petersburg ya Urusi. Austria Vienna ina miadi na Atletico Madrid , na Celtic itakuwa kibaruani na Ajax Amsterdam ya Uholanzi katika kundi H, ambapo pia AC Milan inaikaribisha nyumbani Barcelona.
Michezo hiyo inaendelea siku ya Jumatano ambapo mabingwa Bayern Munich inawakaribisha Pilsen ya Denmark na Leverkusen wako nyumbani kuikaribisha Schachtar Donetzk ya Ukraine.
Watani wa jadi
Huko mjini Dar Es Salaam jana kulikuwa na patashika nguo kuchanika katika uwanja wa taifa ambapo mahasimu wakubwa na watani wa jadi Yanga na Simba waliokuwa wakionesha kazi. Simba ilizinduka kutoka kipingo cha mabao 3-0 katika kipindi cha kwanza na kuuweka mchezo huo kuwa suluhu ya mabao 3-3 hadi mpira kumalizika. Nini kilichosababisha Yanga ambayo ilikuwa inawania kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 5-0 msimu uliopita na watani wao hao kushindwa kutimiza nia yao licha ya kuongoza kwa mabao hayo 3 katika kipindi cha kwanza.
Cristiano Ronaldo ama Zlatan Ibrahimovic mmoja wao atakosa kuonekana katika fainali za kombe la dunia mwakani nchini Brazil kutokana na timu zao za taifa kupangwa leo kuamua ni timu gani inayostahili kwenda Brazil. Nafasi nne zimebakia katika bara la Ulaya. Ufaransa imepangwa kuumana na Ukraine , Ugiriki itakwaana na Romania na Iceland ina kibarua na Croatia katika michezo ya mtoano kuwania tikiti hizo nne za mwisho kwa mataifa ya Ulaya. Michezo hiyo itafanyika Novemba 15 na 19.
Watu 16 wanaotokana na ukoo wa waanzilishi wa chama cha kandanda nchini Uingereza FA, wakitokea kutoka New Zealand na Marekani , watahudhuria uzinduzi wa sanamu katika uwanja wa Wembley leo kama sehemu ya sherehe za miaka 150 za chama hicho tangu kuanzishwa.
Chama hicho ambacho ni cha kwanza duniani kuendesha mchezo wa mpira kiliundwa Oktoba 26, 1863 na chakula cha usiku kitafanyika mjini London siku ya Jumamosi kuadhimisha tarehe hiyo chama hicho kilipoundwa.
Tennis.
Uamuzi wa Serena Williams kwamba amefadhaishwa na uchezaji wake katika msimu wa mwaka 2013 unaonesha nia ya mchezaji huyo kutaka kupita kiwango cha mataji 18 ya Grand Slam ambayo Martina Navratilova na Chris Evert wamefikia na kuwania kuifikia rekodi ya Steffi Graf wa Ujerumani ya mataji 22.
Wakati huo huo Rafael Nadal wa Uhispania anashikilia bado nafasi ya kwanza katika orodha ya wachezaji bora wa tennis kwa wanaume kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho la mchezo huo duniani ATP hii leo.
Na kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo jioni ya leo. Jina langu ni Sekione Kitojo , hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman