Bayern yarejea kwa kishindo kileleni katika Bundesliga
18 Machi 2019Tukianza na Bundesliga Bayern Munich imeelekeza hasira yake ya kuondolewa katika kinyang'anyiro cha ligi ya mabingwa barani Ulaya Champions League , na FC Liverpool katikati mwa wiki kwa kuikandika Mainz 05 kwa mabao 6-0 wakati James Rodriguez akisajili seti yake ya kwanza ya mabao matatu katika Bundesliga jana Jumapili na kukiweka kikosi hicho cha kocha Niko Kovac kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi.
Baada ya kukandikwa mabao 3-1 na Liverpool katikati ya wiki katika mchezo wa Champions League katika timu 16 bora , Mainz ilikiona kilichomtoa kanga manyoya katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich.
"Tulionesha kwamba fadhaa iliyotupata kutokana na kipigo dhidi ya Liverpool tumekwisha sahau, ilikuwa muhimu kuchukua hatua;" alisema kocha wa Bayern Niko Kovac.
Bayern na Dortmund ziko sawa katika pointi 60 kila mmoja, lakini kikosi hicho kutoka jimbo la Bavaria kinatofautiana na Dortmund kwa wingi wa magoli. Dortmund iliichapa Hertha Berlin siku ya Jumamosi kwa mabao 3-2 na kuchukua uongozi wa ligi kwa masaa kabla ya Bayern kurejea kileleni jana. Huyu hapa nahodha wa Dortmund Marco Reus.
"Kila mmoja anafahamu tunavyoelewana, lakini haikuonekana kuwa itakuwa hivyo leo hadi katika dakika ya 92. Hatukuweza kuonana. Lakini tuliendelea kujiamini na hatimaye alinipatia pasi sahihi na niliusukuma tu wavuni".
Tulitaka kupambana na kurejea baada ya ushindi wa Dortmund. Michezo mitatu iliyopita ilikuwa ni alama," mshambuliaji wa Bayern Thomas Mueller amesema , baada ya Bayern kutupia nyavuni mabao 17 katika michezo yake mitatu iliyopita.
Frankfurt haijafungwa
Hapo mapema Eintracht Frankfurt, klabu pekee katika Bundesliga ambayo imebakia katika vikombe vya Ulaya , iliendelea kuwania kupata nafasi ya kucheza katika Champions League msimu ujao , kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Nuremberg.
Frankfurt haijafungwa katika michezo yake 13 iliyopita, ikiwa ni pamoja na tisa katika Bundesliga.
Hapo mapema Werder Bremen iliionyesha cha mtema kuni Leverkusen kwa kuishindilia mabao 3-1. Leverkusen inabakia katika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 42 ikipitwa na Frankfurt ambayo iko katika nafasi ya 5 ikiwa na pointi 46.
Schalke 04 baada ya kutengana na kocha wake Domenico Tedesco katikati ya wiki baada ya kubugizwa mabao 7-0 katika Champions League na Manchester City ilimrejesha kocha wake wa zamani Hubb Stevens. Kocha huyo ambaye alipata mafanikio makubwa na Schalke 04 ikiwa ni pamoja na kutwaa kombe la washindi barani Ulaya 1997, hakuweza kuzuwia kuporomoka kwa Schalke siku ya Jumamosi baada ya kuchapwa kwa bao 1-0 dhidi ya RB Leipzig.
Schalke imeporomoka kutoka nafasi ya 13 na sasa inaelea katika nafasi ya 15 , ikiwa na pointi 3 tu zaidi ya timu iliyoko katika nafasi ya kushuka daraja VFL Stuttgart ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 na Hoffenheim siku ya Jumamosi na kufikisha pointi 20.
Ligi ya Bundesliga na nyingine zote za Ulaya zinasimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya kuwania kufuzu kucheza katika kombe la mataifa ya Ulaya.
Ujerumani inapambana na Serbia katika mchezo wa kirafiki siku ya Jumatano ikiwa ni katika mchezo wa kwanza mwaka huu na kocha Joachim Loew analazimika kupata matokeo mazuri baada ya uamuzi wake uliokosolewa kwa kiasi kikubwa hapa Ujerumani baada ya kuwaondoa kikosini wachezaji wakongwe Mats Hummels, Jerome Boateng na Thomas Mueller kutoka Bayern Munich na kuteua makinda katika kikosi chake.Anapaswa hivi sasa kuthibitisha kuwa ni mtu sahihi kwa timu hiyo baada ya miaka 13 akiwa kocha wa Ujerumani.