BEIJING:Uchina yapinga vikwazo dhidi ya Myanmar
4 Oktoba 2007Uchina inapongeza juhudi za mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa zinazolenga kumaliza tatizo la kisiasa nchini Myanmar lililoanza baada ya maandamano ya kudai demokrasia ya wiki jana.Uchina kwa upande wake inasisitiza kuwa ni muhimu kwa utawala wa kijeshi kujizuia kutoshambulia waandamanaji wakiwemo watawa wa Kibudha. Hata hivyo Uchina iliyo na kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa inapinga hatua ya kuiwekea vikwazo Myanmar na kusisitiza ustawi kwanza.
Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Ibrahim Gambari alifanya mazungumzo na kiongozi wa kijeshi wa Myanmar Jenerali Than Shwe aidha kukutana na kiongozi wa upinzani Bi Aung San Suu Kyi alipokuwa katika ziara ya siku nne wiki hii.Mbali na hayo watawa wa kibudha na raia wanaendelea kukamatwa nchini humo.
Nchi ya jirani ya Uchina ni moja ya mataifa wachache wandani wa Myanmar na mshiriki mkubwa wa biashara inatazamiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika uongozi wa kijeshi unaokabiliwa na upinzani mkubwa katika kipindi cha miaka 20.