Belarus yashtumiwa kwa mzozo wa wakimbizi
12 Novemba 2021Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ireland, Estonia na Albania zimemlaumu rais wa Belarus Alexander Lukashenko kwa kuongezeka kwa mzozo huo wa wakimbizi. Mataifa hayo yamesema kuwa yanalaani matumizi mabaya ya binaadamu ambao maisha yao yamewekwa hatarini kwa madhumuni ya kisiasa na taifa hilo la Belarus huku yakidai kuwa taifa hilo linalenga kuvuruga mataifa jirani na mpaka wa Umoja wa Ulaya huku yakifumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea nchini humo.
Mataifa hayo yamesema kuwa mwenendo wa Belarus haukubaliki na kutoa wito wa hatua kali za kimataifa.
Hata hivyo Urusi ambayo ni mshirika wa kikanda wa Belarus imelitetea taifa hilo huku naibu balozi wake katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyanskiy akiwaambia wanahabari kabla ya mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mataifa ya Magharibi yana aina fulani ya mielekeo ya kimaslahi kwa sababu kuleta mada hiyo aliyoitaja kuwa ya aibu kwa Umoja wa Ulaya mbele ya baraza hilo ilihitaji ujasiri. Polyanskiy ameongeza kuwa Belarus na Urusi haziwasaidii wakimbizi na wahamiaji kuingina barani Ulaya.
Lukashenko ameshutumiwa kwa kusafirisha wahamiaji na wakimbizi kuingia Ulaya kutoka mataifa ya Mashariki ya Kati kama vile Iraq. Rais huyo wa Belarus anadaiwa kutumia mbinu hii kuuadhibu Umoja wa Ulaya kwa sababu ya vikwazo vilivyowekwa dhidi yake na mataifa ya Magharibi.
Belavia yawapiga marufu raia wa Iraq, Syria na Yemen kusafiri kuelekea Belarus
Wakati huo huo, shirika la ndege linalomilikiwa na serikali ya Belarus, Belavia, limesema Ijumaa kwamba litawazuia raia wa Iraq, Syria na Yemen kusafiri kwa ndege kutoka Uturuki kuelekea Belarus kwa ombi la mamlaka ya Uturuki huku mzozo huo wa wakimbizi ukiendelea kati ya Belarus na Poland. Umoja wa Ulaya unasema kuwa Belarus inawatia moyo maelfu ya wakimbizi wanaokimbia sehemu mbali mbali zenye vita duniani kujaribu kuvuka mipaka yake na kwamba unaweza kuweka vikwazo vipya dhidi ya Belarus na mashirika ya ndege ya kusafirisha wahamiaji mapema kufikia Jumatatu.
Umoja huo umeishtumu Belarus kwa kuanzisha mashambulizi huku mshirika wake Urusi ikionya kuwa mzozo huo huenda ukaongezeka kuwa makabiliano ya kijeshi. Shirika la ndege la Belavia ambalo limezuiwa kusafiri kueleka mataifa ya Umoja wa Ulaya baada ya ndege yake kupigwa marufuku kupaa mapema mwaka huu, inaendeleza safari zake katika mataifa kama Misri, Jordan, Armenia, Gorgia, Azerbaijan, Uzbekistan na Kazakhstan.