1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubalozi wa Marekani wafunguliwa upya Cuba

Mjahida14 Agosti 2015

Bendera ya Marekani imepandishwa katika ubalozi wa nchi hiyo nchini Cuba wakati wa ziara ya kihistoria ya Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry.

https://p.dw.com/p/1GFmW
Bendera ya Marekani ikipandishwa nchini Cuba
Bendera ya Marekani ikipandishwa nchini CubaPicha: Reuters/M. Monsivais

Sherehe hiyo ya kupandisha bendera ya Marekani katika ubalozi wa nchi hiyo kwa muda wa miaka zaidi ya 50 inakuja takriban wiki nne baada ya Marekani na Cuba kufufua mahusiano yao ya kibalozi na kuimarisha mipango ya kidiplomasia katika balozi zao.

Katika sherehe hiyo Waziri wa mambo wa nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema kufunguliwa upya kwa ubalozi wa marekani nchini humo kutawanufaisha raia wa Cuba na Marekani.

Katika hotuba yake Kerry amepongeza juhudi za rais wa Cuba Raul Castro na mwenzake wa Marekani Barack Obama kwa kuchukua hatua ya kijasiri ya kutokubali kuwa wafungwa wa historia, na kuangalia mafanikio ya maisha ya leo na kesho.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters/P. Monsivais

Waziri Kerry ameihimiza Cuba kutafuta demokrasia ya kweli huku akisema Marekani haitasita kuhimiza mabadiliko katika taifa hilo la kikomunisti.

Cuba inatarajia Marekani kuiondolea vikwazo vya kiuchumi

Cuba sasa, inaitaka Marekani kusitisha vikwazo vya uchumi vilivyowekwa kwa nchi hiyo, kurejesha kambi ya jeshi la majini la Marekani mjini Guantanamo Bay Mashariki mikononi mwa Cuba na kusimamisha matangazo ya redio na televisheni yanayoingia Cuba. Marekani nao wataihimiza Cuba kuzingatia haki za binaadamu, kurejea kwa wakimbizi na kutaka mali ya wamarekani iliyoingizwa katika mali ya kitaifa na serikali ya Fidel Castro.

Kerry, ambaye ni Waziri wa kwanza wa mambo ya nchi za nje wa Marekani kutembelea nchi hiyo baada ya mika 70, ameandamana na wafanyabiashara, wanachama wa bunge la Congress na wanajeshi wa tatu wa jeshi la majini la Marekani, waliyoishusha bendera ya Marekani nchi Cuba mnamo januari mwaka wa 1961.

Mahusiano ya Marekani na Cuba yalididimia zaidi mwaka wa 1959 wakati wa mapinduzi ya Cuba.

Jumba la Ubalozi wa Marekani nchini Cuba
Jumba la Ubalozi wa Marekani nchini CubaPicha: Reuters/A. Meneghini

Awali Waziri John Kerry aliiambia televisheni moja nchini marekani kabla ya kuondoka kuelekea Havana kwamba anatumai kuona mabadiliko yakianza kutekelezwa. "Watu wengi zaidi wataweza kusafiri, kutakuwa na biashara zaidi, familia nyingi zaidi zitaungana pamoja na natarajia serikali ya Cuba itafanya maamuzi yatakayoanza kubadilisha mambo," alisema Kerry.

Katika ziara hiyo Waziri Kerry anatarajiwa kukutana na wapinzani katika ubalozi wa Marekani mjini Havana. Wapinzani hao hawakualikwa katika sherehe hii ya kupandisha bendera ya Marekani katika ubalozi wake mjini humo kufuatia serikali ya Cuba kuwaona kama vibaraka wa Marekani.

Muandishi: Amina Abubakar/AFP /Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel