1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia yaionya Tanzania

31 Januari 2019

Ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia imesema Tanzania inaweza kujiimarisha zaidi kiuchumi iwapo itachukua hatua za kuwaendeleza wasichana kielimu na kumaliza tatizo la ndoa za utotoni.

https://p.dw.com/p/3CWtD
Tansania Schülerinnen
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia imesema Tanzania inaweza kunufaika zaidi kiuchumi iwapo itachukua hatua za kuwaendeleza wasichana kielimu na kukomesha tatizo la ndoa za utotoni. Imesema, hatua hizo pia zitaweza kuchangia kuchochea maendeleo na kukabiliana na umasikini nchini humo.

Kulingana na ripoti hiyo, kinyume na hapo kuendelezwa kwa ndoa za utotoni na kukosekana kwa elimu kwa wasichana huenda kukachangia kupunguza kipato cha wanawake, hatari za kiafya, kuongezeka kwa unyanyasaji kutoka kwa wenza wao, ongezeko kubwa la idadi ya watu na ongezeko la umasikini, haya yakiwa ni miongoni tu mwa matokeo ya kushindikana kukabiliana na changamoto hizo.

Ripoti hiyo iliyopewa jina "Nguvu ya uwekezaji kwa msichana" ambayo ni ya 11 iliyozungumzia hali ya sasa ya uchumi nchini humo iliyotolewa jana, imeonyesha kwamba licha ya kupungua kwa vitendo kama hivyo dhidi ya wasichana, lakini bado takriban mmoja kati ya wasichana watatu huolewa kabla ya kufikisha miaka 18 ama kwa makubaliano rasmi au yasiyo rasmi.

Lakini pia angalau msichana 1 kati ya wanne hupata mtoto kabla ya kufikisha umri huo wa miaka 18. Kwa sehemu hii bado ni sababu kiwango cha wasichana wanaohitimu elimu ya sekondari nchini humo kusalia kuwa chini.

Pakistan Bildungslücken im Land
Wasichana wengi bado wanakosa fursa ya elimu nchini Tanzania kutokana na ndoa za utotoni.Picha: Reuters/C. Firouz

"elimu sio tu ni uwekezaji kwa msichana, bali pia kwa mtoto wake - kizazi kijacho -na kuleta faida kubwa kwa jamii na uchumi. Ushahidi kwenye ripoti hii unaonyesha wazi thamani ya Tanzania kuwekeza kwa  wasichana na kuondoa ndoa za watoto" amesema Bella Bird, mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Burundi na Somalia.

Moja ya faida kubwa za kiuchumi iwapo ndoa za utotoni zitaondolewa na kumuelimisha mtoto wa kike ni kupungua kwa ongezeko la idadi ya watu lakini pia kuimarisha hali ya maisha na kupunguza umasikini. Kulingana na ripoti hiyo, Tanzania inaweza kuzalisha Dola bilioni 5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030, lakini iwapo ongezeko la idadi ya watu litapungua.

Faida nyingine kubwa ya kiuchumi ya kukomesha ndoa za utotoni inahusisha zaidi kipato cha wanawake, lakini iwapo tu wanawake watapatiwa elimu ya juu. "Iwapo wanawake walioolewa wakiwa wasichana wangeweza  kuchelewesha ndoa zao, kipato chao cha mwaka hii leo kingekuwa kimeongezeka kwa zaidi ya dola milioni 600. Kumaliza tatizo la ndoa za utotoni na kumuelimisha mtoto wa kike si tu ni kitu kizuri kukifanya, lakini pia ni uwekezaji makini", amesema Quentin Wodon, mchumi kiongozi wa Benki ya Dunia na mwandishi mwenza wa ripoti hii.  

Afrika Kuss und Küsse
Wasichana wa umri kama huu wa kubalehe wanatakiwa kupewa stadi za maisha na elimu ya afya ya uzaziPicha: Imago/Danita Delimont

Hatari ya watoto kufa ama kudumaa kabla ya kufikia umri wa miaka mitano kutokana na ndoa za mapema na mimba za utotoni vinaendelea kugharimu uchumi wa taifa kwa kiasi kikubwa. Kukabiliana na tatizo hili la ndoa za utotoni na kuwawezesha wasichana kielimu kwa upande mwingine kunaweza kukachangia kupunguza manyanyaso wanayoyapata wasichana walioolewa wakiwa na umri mdogo ambao wako katika hatari ya kukabiliwa na unyanyasaji kutoka kwa wenza wao.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti hiyo ya karibuni zaidi ni uwekezaji mkubwa zaidi kwenye elimu ya wasichana, upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wasichana ambao wako nje ya mfumo wa elimu na ambao hawawezi kurudi tena shuleni na kuwawezesha kiujuzi wasichana walio katika umri wa kubalehe pamoja na elimu ya afya ya uzazi.

Wakati ripoti ikionyesha utabiri wa ukuaji usioeleweka hatari zilizopo zinasalia kwa kiasi kikubwa ndani ya udhibiti wa serikali. Hatari zilizopo kubwa ni pamoja na kucheleweshwa kwa maboresho ya kuchochea uwekezaji binafsi na kucheleweshwa kuanzishwa kwa miradi ya miundombinu ya umma. Lakini pia mazingira ya nje yanaongeza kitisho kinachohusiana na kupanda kwa gharama za nishati na mbinyo dhidi ya masoko ya fedha.

Ripoti hii ya 11 ya hali ya uchumi nchini Tanzania ilinufaika na msaada kutoka wakfu wa uwekezaji kwa watoto na taasisi ya kimataifa ya elimu ya Global Partnership for Education. Ripoti hii ni moja ya tafiti kadhaa nchini humo zilizoandaliwa na Benki ya Dunia, inayofuatia tafiti za kikanda na kidunia juu ya matokeo ya kiuchumi yanayoshabishwa na elimu duni kwa wasichana na ndoa za utotoni.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Iddi ssessanga