BERLIN: Data zitakusanywa kusaidia vita dhidi ya ugaidi
2 Desemba 2006Matangazo
Bunge la Ujerumani limeidhinisha utaratibu wa kuanza kuweka data katika hatua ya kupambana na ugaidi.Azma ya utaratibu huo utakaoanza kufanya kazi mwakani,ni kuwasaidia polisi na mawakala wa upelelezi kuratibu kazi zao.Mpango huo utaorodhesha majina na habari zitakazosaidia kuwatambua washukiwa.Wakati huo huo bunge limerefusha muda wa sheria ya kupiga vita ugaidi iliyopitishwa baada ya kutokea mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani,Wolfgang Schäuble amesema,nia ni kuhifadhi usalama kama iwezekanavyo kibinadamu,wakati huu wa hatari. Upande wa upinzani lakini una hofu kuwa haki za kutoingiliwa za raia zitakiukwa.