Berlin: Merkel, Hollande, Putin kuzijadili Ukraine na Syria
19 Oktoba 2016Mwenyeji wa mazungumzo hayo Kansela Angela Merkel alisema mazungumzo hayo ambayo yanazihusisha pia Ufaransa na Ukraine, katika mkutano wa kwanza wa pande nne baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja, yanalenga kutoa tathmini ya kweli kuhusu hatua zilizopigwa katika utekekezaji wa mkataba wa amani wa Minsk kwa ajili ya Ukraine.
Mkutano huu unakuja siku moja baada ya ikulu ya Kremlin kutangaza kuwa vikosi vya anga vya Urusi na Syria vimesitisha mashambulizi mjini Aleppo kuekelea kile ilichokiita "usimamishaji kwa misingi ya kibinadamu", hatua ambayo Moscow ilisema imeonyesha nia njema waliyo nayo. Ni tangazo lililokaribishwa na Umoja na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Ulaya, ambao hata hivyo ulisema muda wa usitishaji ulitakiwa kuwa mrefu zaidi kuwezesha ufikishaji misaada.
Merkel alisema yeye pamoja na rais wa Ufaransa Francois Hollande wataijadili Syria na rais Putin kandoni mwa mkutano huo ambao ni makhsusi kwa ajili ya Ukraine, lakini alitahadharisha juu ya matarajio ya miujiza. Alisema hata hivyo kwamba vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na matendo yake nchini Syria vinapwswa kuendelea kuwa njia mojawapo ya kushinikiza nchi hiyo
"Hatutarajii miujiza"
"Ni wazi kwamba katika muktadha wa mkutano kama huu, rais wa Ufaransa na mimi mwenyewe, tuatumia fursa kuzungumza na rais wa Urusi kuhusu hali nchini Syria. Tayari nimefanya hivyo kwa mapana katika mkutano wa kilele wa G20 mjini Hangzhou - na rais wa Ufaransa pia amefanya hivyo.
Hali imekuwa ya maafa zaidi zaidi, kuhusiana na hali ya kibinaadamu, na hii pia ni kwa sababu ya mashambulizi ya Syria na Urusi dhidi ya watu wasiojiweza, hospitali na madakatari," alisema Merkel.
Merkel na Hollande wamekosoa vikali uungaji mkono wa Urusi kwa vikosi vya rais wa Syria Bashar al-Assad. Merkel alisema pia kwamba kipaumbele kwa wakati huu ni "kwamba tuangalie uwezekano wa kupunguza mateso ya watu kwa njia fulani na kulitaja hilo kuwa suala katika mkutano huo unaofanyika Jumatano jioni. Aliyasema hayo katika mkutano wa pamoja kwa waandishi wa habari na rais wa Panama Juan Carlos Varela.
Vikwazo kuendelea kuzingatiwa
"Maoni yangu ni kwamba hakuna njia, ikwemo ile ya vikwazo, inaweza kuondolewa mezani kwa kuzingatia hali ilivyo Syria, lakini kipaumbele ni kwamba tuangalia namna ya kupunguza mateso ya watu kwa njia fulani. Pia katika hili hatutarajii miujiza,lakini mazungumzo ni muhimu wakti wote, hata wakati mitazamo inatofautiana sana," aliongeza kansela huyo wa Ujerumani.
Mkutano huu wa Berlin unafanyika katika mkesha wa mkutano mkuu wa kilele wa viongozi wa mazaifa ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuhusu uhusiano na Urusi, ikwemo vikwazo kuhusiana na Ukraine, ambavyo vitahitaji kurefushwa tena miwshoni mwa mwaka huu.
Mkutano huo wa siku mbili mjini Brussels unatrajiwa pia kuzungumzia mchango wa Urusi nchini Syria, suala ambalo lilizusha mvutano wa hasira kati ya Urusi na Ufransa wiki iliyopita, na kumlaazimu Putin kufuta ziara yake mjini Paris.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,aptn
Mhariri: Oummilkheir Hamidou