Biashara ya kuwauza watu inazidi kuota mizizi
11 Oktoba 2007Mkutano wa siku mbili uliojadili juu ya biashara ya kuwauza watu na maswala ya jinsia uliodhaminiwa na Ureno ambayo ndio inashikilia uenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya umemalizika mjini Porto kaskazini mwa Ureno kwa kauli inayozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua za haraka zitakazo wasaidia wahanga wa biashara ya kuwauza watu.
Azimio lililopitishwa katika mkutano huo linazihimiza nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuharakisha sheria zitakazo shughulikia maswala ya biashara ya kuwauza watu.
Sehemu zinazoathirka zaidi na biashara hiyo ni bara la Afrika, Ulaya Mashariki, Ulaya ya Kusini Mashariki, nchi ambazo zamani zilikuwa chini ya utawala wa Kisovieti, Latin Amerika na nchi za Caribbean.
Sehemu ambazo hasa wahanga hao wanapelekwa ni Marekani, Ulaya Magharibi, Israel, Japan, Thailand na Uturuki.
Ripoti mpya ya shirika la maendeleo la umoja wa mataifa UNDP imesema kwamba biashara ya kuwauza watu inawaingizia wafanya biashara haramu takriban kiwango cha dola bilioni 5 hadi saba kwa mwaka.
Mashirika ya kimataifa yaliyofanya uchunguzi huo yamesema kila mwaka takriban watu laki nane hadi watu milioni moja nukta mbili kote duniani wanauzwa.
Asilimia 80 kati ya watu hao ni wanawake na nusu ya idadi hiyo ni watoto.
Watu hao hutumikishwa katika biashara ya ukahaba.
Wanawake wengi wasiokuwa na elimu hutumbukia katika mtego wa wafanyabiashara haramu ya kuwauza watu.
Wawakilishi katika mkutano uliofanyika mjini Porto ambao pia ulihudhuriwa na watalaamu kutoka nje ya nchi za Umoja wa Ulaya walijadili mbinu mbali mbali zinazotumika kuwashawishi watu.
Kwa mfano wafanya biashara hao huwapa wahanga vyeti vya kusafiria na fedha ambapo wahanga wengi hudanganywa na kuamini kuwa wanapelekwa kufanya kazi za usanii au kazi za kuwalea watoto na mara nyingine huambiwa wazi kuwa wanakwenda kufanya kazi ya ukahaba lakini hawaelezwi ukweli kuwa watakabiliwa na mikataba ya kitumwa.
Ripoti kuhusu wanawake wanaotumikishwa katika biashara ya ukahaba nchini Ureno iliwasilishwa katika mkutano huo.
Imedhihirika kwamba wanawake kutoka Brazil na Nigeria ndio wanaohusishwa zaidi katika biashara hii haramu nchini Ureno.
Wanawake hao ambao huibiwa na kuletwa nchini Ureno hatimae hugeuka na kuwa ndio mawakala wa kuwaingiza wanawake wengine kwenye maovu hayo kutoka katika nchi zao.
Wakati huo huo makundi haya ya Kimafia yaliyokuwa na ushawishi mkubwa huko Ulaya ya Mashariki mnamo miaka ya 90 sasa hayana tena nguvu kwani polisi wameimarisha msako dhidi ya makundi yanayofanya biashara ya kuwauza watu.
Mapendekezo yaliyofikiwa katika mkutano huo wa siku mbili yatawasilishwa mbele makao makuu ya Umoja wa ulaya mjini Brussels huku nchi wanachama wa umoja huo zikijiandaa kuadhimisha siku ya kupambana na biashara ya kuwauza watu tarehe 18 mwezi huu wa Oktoba.