1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bibi Benazir Bhutto wa Pakistan anawalaumu watu wenye siasa kali kujaribu kutaka kumuuwa

19 Oktoba 2007

Katika miripuko mikubwa ya mabomu jana usiku huko Karachi, wakati waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Bibi Benazir Bhutto, akikaribishwa na maelfu ya wafuasi wake wa chama cha People’s alipokuwa akirejea nyumbani kutoka uhamishoni uliodumu miaka minane, si chini ya watu 138 waliuwawa na zaidi ya 300 walijeruhiwa, wengi wao wakiwa katika hali mbaya.

https://p.dw.com/p/C7gs
Bibi Benazir Bhutto akiharakishwa kuingizwa katika gari baada ya kuripuka mabomu yaliokusudiwa kutaka kumuuwa
Bibi Benazir Bhutto akiharakishwa kuingizwa katika gari baada ya kuripuka mabomu yaliokusudiwa kutaka kumuuwaPicha: AP

Hayo yamesemwa leo mjini Islamabad na mkuu wa polisi wa karachi, Azhar Farooqi. Mwenyewe Bibi Bhutto punde hivi aliwahutubia waandishi wa habari na akasema yeye alikuwa anajuwa na alionywa kabla kwamba kutafanywa jaribio la kutaka kumuuwa, lakini ilimbidi ajibu matakwa ya wafuasi wake waliotaka kumuona anarejea nyumbani.

Bibi Bhutto aliwalaumu watu wenye kuendesha siasa kali za utumiaji nguvu kwa kutaka kujaribu kumuuwa na akasema yeye hatasalimu amri kuliwachia taifa kubwa la Pakistan kwa watu hao. Alitaja kwamba walikuwa watu wawili walioripuwa mabomu hayo ya jana, na kwamba walinzi wake walimgundua mtu watatu aliyekuwa na bastola na mwengine aliyekuwa amevaa fulana ilio na baruti.

Bibi Bhutto alisema kabla hajawasili Karachi hapo jana alionywa kwamba kulikuweko na kikosi kimoja cha wauwaji wa mtandao wa al-Qaida, kikosi kingine cha Wataliban, kingine kutoka Wataliban wa Pakistan na pia kikundi kingine cha nne, anaamini kutokea Karachi. Hata hivyo, kichinichini, Bibi Bhutto alilaumu hatua dhaifu za usalama zilizochuliwa na serekali ya Pakistan kumlinda wakati alipowasili:

+Tuliona taa za njiani zimezimwa, na wakati mimi siilaumu serekali kutokana na shambulio hilo la kujitolea mhanga, na wakati mimi siilaumu serekali, wakati huu, kutokana na majaribio hayo ya kutaka kuniuwa, hata hivyo, tunahitaji kufanywe uchunguzi kwa nini taa za barabarani zilizimwa. Kwa masaa yote manne taa za barabarani zilizimwa. Makamo wangu wa rais wa chama alijaribu kuwasiliana na mshauri wa usalama wa taifa, Bwana Tariq Aziz, kumwambia kwamba walinzi wetu wa usalama walikuwa na shida kuwatambua waripuaji wa mabomu ya kujitolea mhanga pamoja na watu waliojificha na wanaofyetua risasi, kwa vile tulikuwa hatuoni. Tulikuwa tunasafiri katika kiza, tulikuwa hatuoni kile kilichokuweko pembeni mwetu. Ni jambo lililokuwa linazuwia usalama wetu. Serekali ilitambuwa kwamba tulihitaji usalama.+

Bibi Bhutto alisema walinzi wake walizuwia kusitokee mauaji zaidi, kwani walisimama kidete na walikizuwia kikosi cha pili cha washambuliaji kilichotaka kulikaribia gari lake. Akionekana mkakamavu, Bibi Bhutto alisema amerejea Pakistan ili kuipatia nchi hiyo demokrasia na maendeleo na kuwazuwia walio na siasa kali wasiwe na usemi.

Lakini hayo ya jana hayajaja kama mshangao mkubwa, kwa wachunguzi wa mambo. Maisha ya Bibi Bhutto yamekumbwa na mitihani na manusura hata kabla ya shambulio la jana. Amewahi kuwa mara mbili waziri mkuu wa nchi hiyo isiokwisha vurugu, na aliingia katika medani ya kisiasa pale baba yake, Zulfiqar Ali Bhutto, aliponyongwa na mdikteta wa kijeshi wa wakati huo, Jenerali Zia-ul Haq. Baba yake, ambaye aliweka misingi ya Pakistan kuwa dola ya kinyukliya, alipinduliwa kutoka madarakani na Jenerali Zias ul-Haq ambaye alimwachia auliwe kwa kitanzi, licha ya malalamiko kutoka duniani kote.

Zia ul-Haq aliendesha siasa kali za Kiislamu katika Pakistan hadi pale alpokufa kutokana na ajali ya ndege hapo mwaka 1988. Benazir Bhutto, licha ya kuwa na doa la madai ya kula rushwa alipokuwa madarakani, bado anaungwa mkono na watu wengi, hasa mamilioni ya wakaazi maskini wa mijini na mashambani.

Hatua ya karibu ya Benazir kufanya mashauriano na mtawala wa sasa wa kijeshi, Rais Pervez Musharraf, imelaumiwa vikali na watu wengi, lakini yeye anashikilia kwamba nia yake ni kuweko kipindi cha amani cha mpito kutoka utawala wa kijeshi. Na watu wengi waliojitokeza jana kumpokea huko Karachi wamedhihirisha anaungwa mkono na watu wengi. Huenda akashinda katika uchaguzi ujao wa bunge, na kuwa waziri mkuu kwa mara ya tatu hapo Januari mwakani, lakini mustakbali wake hauna uhakika; wako watu wanaotaka kumuuwa na pia wanajeshi wa vyeo vya juu hawamuangalii kwa jicho zuri.