Biden akutana na Ghani, Abdullah kuhusu Afghanistan
25 Juni 2021Mkutano huo kwenye Ikulu ya Marekani unaweza kuwa muhimu kwa Ghani na kwa utawala wa Biden kama ishara ya kuthibitisha uungani mkono wa Marekani kwa kiongozi wa Afghanistan anayepambana sasa na uasi wa kundi la Taliban, ambalo linaonekana kusonga mbele, mashambulizi ya mabomu na mauaji ya watu mashuhuri, huku pia maambukizo ya COVID-19 na vita vya kisiasa vikiimarika nchini mwake.
Balozi wa zamani wa Marekani nchini Afghanistan, Ronald Neumann, amesema kitendo cha Biden kumualika Ghani mjini Washington ni ujumbe kwamba anamuunga mkono, hasa katika hali ambapo kiwango cha hamasa kimetikisika na mambo yanaelekea kuharibika kutokana na uamuzi wa Marekani kuondowa wanajeshi wake wote ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Hata hivyo, mazungumzo ya leo (Juni 25) yanafanyika ikiwa ni miezi michache baada ya maafisa wa Marekani kumshinikiza Rais Ghani kuachia madaraka na kuipisha serikali ya mpito chini ya makubaliano ya kisiasa waliyoyabuni kuvunja mkwamo wa kisiasa nchini Afghanistan.
Wanajeshi wa Marekani hawatabakia
Huenda ndio sababu Ghani amealikwa pamoja na hasimu wake mkuu kisiasa, Abdullah Abdullah, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa Baraza Kuu la Muafaka wa Kitaifa.
Biden atatumia mkutano wa leo kuwataka wawili hao kuungana kwa dhati na atathibitisha uungaji mkono wa Marekani kwa makubaliano ya amani, amesema Jean-Pierre, afisa habari wa Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, maafisa wa Marekani wameweka wazi kwamba kamwe Biden hatasimamisha uamuzi wa nchi hiyo kuondowa wanajeshi wake nchini Afghanistan, mchakato unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa Julai ama mwanzoni mwa mwezi wa Agosti mwaka huu.
Na licha ya kundi la Taliban kuendelea kupata mafanikio dhidi ya vikosi vya serikali, Biden pia haonekani kutangaza msaada wa kijeshi wa Marekani kuwazuwia wanamgambo hao kusonga mbele.
Badala yake, rais huyo wa Marekani ameliomba baraza la Congress kuidhinisha msaada wa dola bilioni 3.3 kwa masuala ya usalama nchini Afghanistan na kwa sasa anapeleka dozi milioni 3 za chanjo kusaidia vita dhidi ya COVID-19.