Biden aongoza majimbo mengi zaidi uchaguzi wa Democratic
4 Machi 2020Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden ameshinda katika majimbo makubwa tisa katika Jumanne maalumu "Super Tuesday" wakati mpinzani wake wa karibu Bernie Sanders akiwa na majimbo sita upande wake. Matokeo hayo katika kura hiyo ya mchujo, yamerejesha matumaini ya Biden kuweza kukiwakilisha chama chake cha Democratic katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi Novemba.
Biden ameshinda katika majimbo tisa kati ya 14 na kujizolea kura nyingi katika jimbo muhimu la Texas. Ameshinda pia kwenye majimbo ya Minesota, Alabama, Tennessee, Oklahoma, Arkansas, North Carolina, Virginia, Texas, na Massachuessets.
Ushindi huo wa jana unampa nafasi ya kuweza kuchaguliwa kukiwakilisha chama cha Demokratic atakapochuana na Rais Donald Trump mwezi Novemba.
Kwa upande wake Bernie Sanders, mfuasi wa siasa za mrengo wa shoto alishinda kwenye jimbo lake la nyumbani Vermot, Colorado, Utah na California. Licha ya kupitwa na Joe Biden katika chaguzi za jana, Sander alikuwa na matumaini alipozungumza na wafuasi wake.
Katika kinyang'anyiro hicho Meya wa zamani wa jiji la New York, Meya Michael Bloomberg, hakupata ushindi katika jimbo jingine zaidi ya eneo la American Samoa, lililo kwenye bahari ya Pacific. Rais Trump ambaye alikuwa akifuatilia matokeo kwa njia ya Televisheni aliandika ujumbe wa kejeli kwa njia ya Twitter akimkosoa mgombea Elizabeth Waren kwa kushindwa kupata ushindi hata katika jimbo lake la nyumbani la Massachusetts. Biden aliujibu ujumbe huo kwa kuandika "Njoo Novemba, tunakwenda kukushinda!"
Upigaji kura kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi Machi
Chama cha Democratic kitaendelea na upigaji kura katika majimbo yaliyosalia huku majimbo 11 zaidi yakitarajiwa kupiga kura kufikia mwishoni mwa mwezi Machi. Majimbo hayo ni pamoja na Idaho, Michigan, Mississippi, Missouri, North Dakota Washington.
Wakati kura zilipokuwa zikipigwa hapo jana Vimbunga vikali viliathiri vituo vya kupigia kura katika jimbo la Tennessee wakati hofu ya virusi vya corona ikiviacha baadhi ya vituo vya kupigia kura katika mjimbo ya California na Texas bila wafanyakazi wa kutosha.
Vimbunga hiyo vimewauwa watu 25 na kuharibu majengi 140 jimboni humo. Upigaji kura katika jimbo hilo uliongezwa muda kwa saa moja kutokana na changamoto hiyo ya vimbunga.