1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden asisitiza ana uwezo mzuri wa kukumbuka matukio

9 Februari 2024

Rais Joe Biden wa Marekani amesema, madai yaliyotolewa na mwanasheria maalum Robert Hur, kuwa rais huyo ana uwezo mdogo wa kukumbuka ni uongo mtupu.

https://p.dw.com/p/4cDNp
Rais wa Marekani Joe Biden anatafuta kuongoza kwa muhula wa pili wa miaka minne
Joe Biden hatokabiliwa na mashitaka ya jinai kwa kuzihifadhi nyaraka za siri alipoondoka katika wadhifa wa makamu wa rais 2017Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Biden ametoa kauli hizo katika kujibu ripoti ya mwanasheria Hur inayofuatia uchunguzi wa miezi 15 juu ya kutunzwa vibaya kwa nyaraka za siri. Rais huyo wa Marekani hakupatikana na hatia.

Uchunguzi huo uligundua kuwa Rais Biden alizihifadhi kwa makusudi na kuzisambaza taarifa za siri wakati alipokuwa raia wa kawaida, zikiwemo kuhusu sera ya kijeshi na mambo ya nje nchini Afghanistan, lakini ripoti hiyo imebaini kuwa kuwa hakuna mashtaka ya jinai yanayopaswa kufunguliwa. "Kama mnavyojua, mwanasheria maalum alitoa matokeo yake leo kuhusu uchunguzi wao katika utunzaji wangu wa nyaraka za siri. Nilifurahi kuona alifikia uamuzi madhubuti - kwamba hakuna mashtaka yoyote yanayopaswa kuwasilishwa dhidi yangu katika kesi hii."

Robert Hur akizungumza katika kikao cha waandishi habari mjini Washington 2017
Mwanasheria Robert Hur alisema Biden hana hatiaPicha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Ripoti ya Hur yenye kurasa 388 iligusia mada mbalimbali ikiwemo suala la uwezo wa Biden kukumbuka mambo. Biden alionekana mwenye hasira wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington DC kuhusu kujumuishwa katika ripoti hiyo kwa marehemu mwanawawe Beau aliyefariki dunia kwa kuugua saratani. "Ninajua kuna umakini fulani uliowekwa kwa lugha fulani katika ripoti kuhusu jinsi nnavyoyakumbuka matukio. Hata imeandikwa kuwa sikumbuki wakati mwanangu alifariki. Vipi anaweza kuthubutu kuibua hilo? Kwa kweli nilipoulizwa swali hilo nilijiwazia: ‘Hilo kwa kweli linawahusu nini?

Kesi hiyo ilionekana kufananishwa na ya Rais wa zamani Donald Trump aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kwa madai ya kuzikusanya na kuzitunza nyaraka za siri katika makazi yake ya Mar-a-lago jimboni Florida na kukataa kuzirejesha kwa serikali. Trump, mara moja ameitumia ripoti hiyo ya mwanasheria maalum kujionyesha kuwa mwathiriwa wa mfumo wa sheria wenye ngazi mbili. Kumaanisha unawapendelea baadhi ya watu.

Shirika la ujasusi la Marekani FBI lilipekua makazi ya Biden mwaka wa 2022
Nyaraka za siri zilipatikana katika gaerji ya BidenPicha: Justice Department/AP/picture alliance

Hur, alisema kulikuwa na tofauti kadhaa za wazi kati ya kesi za Trump na Biden, akibainisha kuwa Trump alikataa kurejesha nyaraka za siri kwa serikai na akadaiwa kuwa alizuia uchunguzi kufanywa, wakati Biden alizikabidhi kwa makusudi.

Kuhitimishwa kwa kesi hiyo kunahakikisha kuwa Biden, tofauti na mpinzani wake wa urais anayetarajiwa katika uchaguzi wa 2024 Donald Trump, hatapewa kifungo jela kwa kuzitunza vibaya nyaraka nyeti za serikali. Lakini kunasababisha aibu zaidi kwa Biden aliye na umri wa miaka 81, kuwa mtu mzee zaidi kuwahi kuhudumu kama rais wa Marekani anayejaribu kuwashawishi wapiga kura kuwa anapaswa kuhudumu kwa muhula mwingine wa miaka minne.

afp, dpa, ap, reuters