Biden kumteua Merrick Garland kuwa mwanasheria mkuu
7 Januari 2021Jaji Garland, ambaye kwa sasa ni jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Washington, alipata umaarufu mwaka 2016 wakati ambapo rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alimteua kuwa jaji wa Mahakama ya Juu kuziba nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha jaji Antonin Scalia. Hata hivyo, uteuzi huo ulipingwa na wabunge wa chama cha Republican ambao walikuwa wanadhibiti Baraza la Seneti.
Katika taarifa yake, Biden amesema Garland atasaidia kurejesha uhuru wa idara ya mahakama, ili ihudumie maslahi ya wananchi na sio rais, kurejesha tena imani ya umma katika utawala wa sheria na kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha mfumo wa mahakama unakuwa wa haki na sawa.
Viongozi waendelea kulaani vurugu
Wakati hayo yakijiri, viongozi mbalimbali duniani wameendelea kulaani vurugu zilizotokea siku ya Jumatano katika majengo ya bunge mjini Washington, Marekani, baada ya wafuasi wa Rais Donald Trump kufanya uvamizi huo. Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amesema matukio ya jana ni matokeo ya uongo wa kuigawa na kuidharau demokrasia, matokeo ya chuki na kuamsha hasira kwa kiwango cha juu kabisa.
''Hili lilikuwa shambulizi katikati ya demokrasia ya Marekani, shambulizi ambalo limeyagharimu maisha ya watu wanne. Taswira hiyo imetushtua na imetuonesha jinsi hata demokrasia kongwe na yenye nguvu zaidi ulimwenguni ilivyo hatarini,'' alifafanua Steinmeier.
Makamu wa zamani wa Rais wa Nigeria, Atiku Abubakar amesema vurugu za Marekani ni fundisho tosha kwamba taasisi zenye nguvu na sio haiba kubwa ya mtu ndiyo kizingiti cha utajiri wa utamaduni wa kidemokrasia.
Viongozi wengine waliolaani vurugu za Marekani ni pamoja na Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, Rais wa Slovakia, Zuzana Caputova na Katibu Mkuu wa Jumuia ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg.
Maafisa wanajiuzulu
Ama kwa upande mwingine, mjumbe maalum wa Trump huko Ireland Kaskazini, Mick Mulvaney amejiuzulu kutokana na vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Trump. Mulvaney aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi wa Ikulu ya Marekani ameongeza idadi ya maafisa wa utawala wa Trump wanaojiuzulu kutokana na ghasia hizo.
Mara baada ya vurugu hizo, ambazo hadi sasa Trump ameshindwa kuzilaani, naibu mshauri wa usalama wa taifa, Matt Pottinger alijiuzulu. Aidha, Stephanie Grisham, aliyekuwa katibu wa habari wa Ikulu ya Marekani pia ametangaza kujiuzulu. Grisham kwa sasa alikuwa msemaji wa mke wa rais Trump, Melania Trump.
(AFP, AP, DPA, Reuters)