1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Ruto kujadili msamaha wa deni kwa Kenya wiki hii

21 Mei 2024

Mazungumzo ya Rais Biden na Rais Ruto siku ya Alhamisi yatajikita kwenye uhusiano wa nchi zao kibiashara na kiusalama, msamaha kwa madeni ya Kenya miongoni mwa mengine.

https://p.dw.com/p/4g5zs
Kenya/Marekani | Rais wa Kenya William Ruto akiweka shada la maua kwenye makaburi ya Martin Luther King Jr na Corett Scott King
Rais wa Kenya William Ruto na mkewe Rachel Ruto (kushoto) na Bernice King, mwanaye Martin Luther King Jr. na Corett Scott King. Hii ni baada ya kuweka shada la maua kwenye makaburi ya wazazi wa Bernice King.Picha: John Bazemore/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Rais wa Kenya William Ruto anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington wiki hii na miongoni mwa masuala makuu yanayotarajiwa kutawala mazungumzo yao ni pamoja na mzozo wa Haiti na juhudi za kuimarisha biashara baina ya Kenya na Marekani. 

Ziara hiyo ya Rais William Ruto imetajwa kuwa ya kihistoria ikizingatiwa ndiyo ziara ya kwanza rasmi inayofanywa na rais wa Kenya katika ikulu ya White House ndani ya miongo miwili, na ndiyo ya kwanza kwa kiongozi yeyote wa Afrika tangu mwaka 2008.

Mazungumzo ya Rais Biden na Rais Ruto siku ya Alhamisi yatajikita kwenye uhusiano wao kibiashara na  kiusalama, namna ya kushughulikia madeni ya Kenya, ufadhili wa Kenya, mchango wa Kenya katika kusuluhisha migogoro ya kimataifa ikiwemo Ukraine, Sudan, Haiti na kwingineko.

Kiunzi cha mahakama dhidi ya hatua ya polisi wa Kenya kupelekwa Haiti

Kuhusu Haiti, ahadi ya Kenya ya kuwatuma polisi 1000, kuongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa kurejesha utulivu katika taifa hilo linalozongwa na machafuko ya magenge yenye silaha itakuwa ajenda kuu.
Kuhusu Haiti, ahadi ya Kenya ya kuwatuma polisi 1000, kuongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa kurejesha utulivu katika taifa hilo linalozongwa na machafuko ya magenge yenye silaha itakuwa ajenda kuu.Picha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Soma pia: Marekani imeahidi kutoa dola milioni 100 kwa Haiti

Mataifa kadhaa pia yamekubali kuwapeleka polisi wao Haiti lakini lakini Marekani na Umoja wa Mataifa wamesema hawatapeleka vikosi vyao.

Vyanzo vya Habari vimeliarifu shirika la Habari la AFP kwamba kikosi cha kwanza cha polisi cha Kenya kinatarajiwa kusafiri wiki hii kuelekea mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, umbali wa kilomita 12,000 kutoka Nairobi, licha ya kesi mpya iliyowasilishwa mahakamani kupinga hatua hiyo.

Soma pia: Kenya yakabiliwa na kiunzi kupeleka polisi Haiti

Ruto amekuwa akitetea uamuzi wake kupeleka polisi Haiti akisema ni "ujumbe wa kiutu” katika nchi hiyo maskini ya Magharibi, ambayo imezongwa na umaskini, msukosuko wa kisiasa na majanga ya asili kwa miongo mingi.

Marekani yalenga kukabili ushawishi wa China barani Afrika

Moja kati ya malengo makuu ya Marekani kupanga ziara hiyo ya kitaifa kwa Rais Ruto ni kukabili ushawishi wa China unaozidi kuongezeka barani Afrika.
Moja kati ya malengo makuu ya Marekani kupanga ziara hiyo ya kitaifa kwa Rais Ruto ni kukabili ushawishi wa China unaozidi kuongezeka barani Afrika.Picha: GIANLUIGI GUERCIA/Pool via REUTERS

Mwezi uliopita, afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya fedha ya Marekani Jay Shambaugh alionya China na nchi nyingine ambazo zimekopesha sana nchi za kipato cha chini dhidi ya kuwalimbikizia adhabu zaidi kifedha wanaposhindwa kulipa.

Soma pia: Kenya yasaka mikopo zaidi kutoka China

Afisa mmoja mkuu wa utawala ameliambia shirika la Habari la Reuters kuwa Marekani inazitaka nchi zenye mikopo mikubwa kama China, ambayo ni mkopeshaji mkuu wa Kenya, kuzipa nchi zinazodaiwa unafuu.

Utata wa riba za juu kwa madeni Afrika inapewa

Afisa huyo amesema miongoni mwa yanayotarajiwa kujitokeza kwenye taarifa ya pamoja baada ya mkutano wa Biden na Ruto ni jinsi nchi kama Kenya inaweza kukabili tatizo la madeni.

viongozi wa Afrika walizitaka nchi tajiri kutoa mchango mkubwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa ya Benki ya Ulimwengu, yenye riba ndogo.
viongozi wa Afrika walizitaka nchi tajiri kutoa mchango mkubwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa ya Benki ya Ulimwengu, yenye riba ndogo.Picha: Solomon Muchie/DW

Marekani pia inazihimiza taasisi za kimataifa za kifedha kuzipa nchi zenye mapato ya chini kama Kenya na mataifa mengine mikopo yenye riba nafuu.

Katika mkutano ulioandaliwa na Ruto mwezi uliopita, viongozi wa Afrika walizitaka nchi tajiri kutoa mchango mkubwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa ya Benki ya Ulimwengu, yenye riba ndogo

kituo ambacho mataifa yanayoendelea hutegemea kusaidia kufadhili maendeleo yao na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

AFPE, RTRE