Biden, Zelensky wasaini mkataba wa ´kihistoria´ wa usalama
14 Juni 2024Matangazo
Mkataba huo utakashuhudia Washington ikiupatia utawala mjini Kyiv msaada wa kijeshi na mafunzo kwa muongo mmoja unaokuja.
Halfa ya utiaji saini mkataba huo imefanyika pembezoni mwa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri duniani la G7 uliofunguliwa jana kwenye mkoa wa mwambao wa Italia wa Apulia.
Zelensky ameitaja siku ya utiaji saini mkataba huo kuwa ya kihistoria katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Urusi na kwamba anatumai mafunzo na msaada wa kijeshi wa Marekani utafungua njia kwa hatimaye Ukraine kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Kwa upande wake Rais Biden amesema mataifa ya kundi la G7 yamechukua hatua madhubuti kumwonyesha Rais Vladimir Putin wa Urusi kwamba hatoweza kuushinda mshikamano wa wanademokrasia.