BJP yashinda uchaguzi wa India
16 Mei 2014Waziri Mkuu Manmohan Singh amempigia simu Modi kumpongeza kwa ushindi wa chama chake cha Bharatiya Janata (BJP). Hiyo ni baada ya matokeo ya awali kuonesha kuwa chama hicho na washirika wake tayari wameshajizolea zaidi ya idadi ya viti 272 vinavyohitajika kuwa na wingi wa kutosha kwenye bunge la nchi hiyo lenye viti 543.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi, Modi anaongoza kwenye majimbo yote mawili aliyogombea, Vadodara lililo Gujarat na mji mtakatifu wa Wahindu wa Vanarasi.
Ravi Shankar Prasad, kiongozi BJP katika mji mkuu New Delhi, ameuelezea ushindi wa chama chake kama ujumbe wa kuvunjika moyo wa wapiga kura.
"Watu wamechoshwa na uongozi mbaya ambao umeifanya India kuwa masikini, yenye huzuni na nchi ya mateso. Na nauheshimu uwelewa wa watu wa India hii yenye maumivu kwa namna walivyopiga kura. Sasa matokeo yanaonesha kuwa serikali makini itakayofanya kazi, itaundwa chini ya uongozi wa Narendra Modi." Amesema Prasad.
Congress yaangukia pua
Hadi sasa ni majimbo 50 yaliyothibitika kuongozwa na Congress, lakini baadhi ya viongozi wa chama tawala cha Congress, bado wana matumaini kuwa chama chao kitaendelea angalau kushikilia baadhi ya viti vyake, hata kama si kuendelea kutawala.
"Huu ni muelekeo tu wa matokeo na sio matokeo kamili. Kuna tafauti kati ya masaa machache na nambari na matokeo halisi. Hivyo, tafadhali subiri. Si lazima muelekeo wa matokeo uwe ndio matokeo hasa." Amesema Shobha Oja, kiongozi wa Congress.
Hata kiongozi wa kampeni za chama hicho, Rahul Gandhi, anaongoza kwa ushindi mdogo sana kwenye ngome ya familia yake, jimbo lake la Amethi, ambalo limewahi kushikiliwa na ami, baba yake Rajiv na mama yake, Sonia, kwa vipindi tafauti. Kulipoteza jimbo hili kutakuwa hasara kubwa kwa kirembwe hicho cha kiongozi wa uhuru wa India.
Waziri Mkuu mpya Narendra Modi
Ikiwa muelekeo wa matokeo haya ya awali utakwenda kama ulivyo, basi BJP watakuwa na wingi wa kutosha kwa kuwa na zaidi ya viti 272 katika Lok Sabha, au Baraza la Wawakilishi.
Matokeo haya yatamfungulia njia Modi, mwenye umri wa miaka 63, kuwa waziri mkuu na kuwatangaza wanasiasa wanaomtii kwenye nafasi muhimu katika baraza la mawaziri: fedha, mambo ya ndani, ulinzi na mambo ya nje.
Lakini ikiwa Modi atashindwa kupata wingi wa kutosha, atalazimika kuingia kwenye mazungumzo marefu ya kuunda serikali ya mseto na vyama vya majimbo, jambo ambalo litautia rehani utiifu wa kisiasa na yumkini kuilainisha ajenda yake ya mageuzi, aliyoiuza kwa wapiga kura wakati wa kampeni.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman