1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blair aelekea Jordan, Israel na Palestina

Mohammed AbdulRahman23 Julai 2007

Ni ziara ya kwanza katika eneo hilo tangu alipochaguliwa kuwa mjumbe maalum wa mashariki ya kati na kundi la pande nne linalosaka amani kati ya Israel na wapalestina

https://p.dw.com/p/CHAk
Tony Blair,mjumbe maalum wa Mashariki ya kati kwa niaba ya pande nne zinazosaka amani kati ya Israel na wapalestina.
Tony Blair,mjumbe maalum wa Mashariki ya kati kwa niaba ya pande nne zinazosaka amani kati ya Israel na wapalestina.Picha: AP

Ziara ya Bw Tony Blair ni sehemu ya hatua kadhaa za kibalozi zenye lengo la kuufufua mwenendo wa amani. Kituo cha kwanza cha ziara yake ni Jordan hii leo na baadae ataelekea Israel na Ukingo wa magharibi kesho(Jumanne).

Chini ya masharti ya kibali alichopewa kutokana na uteuzi wake, Blaie hapaswi kuzungumza na chama cha Hamas, ambacho kimeorodheshwa na Marekani iliyompigia debe katika uteuzi huo,kuwa kundi la kigaidi na ambacho sasa kinalidhibiti eneo la Gaza baada ya mapambano yaliomwaga damu na hasimu yake chama cha Fatah cha Rais Mahmud Abbas,

Kundi hilo la pande nne, Umoja wa mataifa, umoja wa Ulaya, Marekani na Urusi, limekua likijaribu tangu 2003 kutekeleza mpango unaojulikana kama “ramani ya kuelekea amani” kati ya Israel na wapalestina. Lakini waraka huo umeshindwa kufikia lengo la kuundwa taifa la Palestina litakaloishi kwa amani pamoja na Israel. Lengo hilo lilikua lifikiwe 2005.

Hali hiyo ikamsababisha aliyekua mjumbe maalum wa kundi hilo , Rais wa zamani wa Benki ya dunia James Wolfensohn akajiuzulu akivunjwa moyo na kukwama kwa utaratibu huo wa kusaka amani.

Akiwa mjini Amman Jordan, Bw Blair atajadiliana na Waziri wa mambo ya nchi za nje Abel Illah Khatib juu ya njia za kuufufua urataibu huo wa amani. Kesho alasiri ataonana na rais wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah na baadae na Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert mjini Jerusalem.

Wiki iliopita Blair alisema ana matumaini kutapatikana mabadiliko katika mwenendo huo wa amani kati ya Israel na wapalestina.

Ziara yake ya kwanza katika eneo hilo akiwa mjumbe maalum wa kundi hilo la pande nne, inafuatia mazungumzo yake mjini Lisbon na waakilishi wa ngazi ya juu ya kundi hilo ambapo akizungumza baadae alisema “ amani inawezekana na amejizatiti kuleta mabadiliko.

Wakati huo huo katika hatua nyengine ya juhudi za kibalozi, spika wa bunge la Israel Bibi Dalia Itzik alifanya ziara ya kushangaza nchini Jordan jana kwa mazungumzo tafauti na Rais wa palestina Abbas na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jordan hakuna taarifa iliotolewa baada ya mazungumzo yao, lakini hapo awali msemaji wake alisema mazungumzo yangetuwama juu ya njia za kufufua haraka jitihada za kuleta amani katika eneo hilo.

Mnamo siku ya Jumatano, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jordan na mwenzake wa Misri Ahmed Abu Gheit wataizuru Israel, kwa niaba ya umoja wa nchi za kiarabu wenye wanachama 22, kuupa msukumo mpango uliowasilishwa na Saudi Arabia.

Umoja huo wa nchi za kiarabu umetoapendekezo kwa Israel la kuwa tayari kurejesha uhusiano wa kawaida na dola hiyo ya Kiyahudi, ili badala yake iondoke katika ardhi zote za waarabu inazozikalia ambazo iliziteka katika vita vya siku 6 , 1967, kuundwa dola huru ya wapalestina na kurudi kwa wakimbizi wa kipalestina.

Wiki iliopita, Rais George W. Bush wa Marekani pia aliwataka washirika wake wa kiarabu, Jordan, Misri na Saudi Arabia, ziijongelee Israel, zimuunge mkono Rais Abbas wa Palestina na zishiriki katika mkutano wa kimataifa kuufufua mwenendo wa amani. Rais Bush atajadiliana juu ya juhudi zake mpya, atakapoonana na Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan kesho, Ikulu mjini Washington.