Blatter aitaka Qatar kuheshimu haki za wafanyakazi
16 Machi 2015Blatter na Mfalme Tamim bin Hamad Al-Thani walifanya mazungumzo ya hapo jana katika Kasri la Al Bahr kabla ya mkutano wa Kamati Kuu ya FIFA unaopangwa Alhamisi na Ijumaa wiki hii ili kuamua kuhusu tarehe za mwisho za Kombe la Dunia la 2022. Dimba hilo litakuwa la kwanza kuwahi kuandaliwa katika mwezi wa Novemba na Desemba kwa sababu ya kiwango cha joto kali nchini Qatar.
Mashirika ya Haki za Binaadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yametoa wito kwa Qatar kuharakisha mageuzi ya mfumo wa ufadhili wenye utata marufu kama “Kafala”, ambao unawawezesha waajiri kuwazuia wafanyakazi wao kuondoka nchini humo au kubadilisha kazi na umefananishwa na utumwa mambo leo.
katika jibu la mkutano wa jana, kiongozi mmoja wa Amnesty, James Lynch amesema “ilikuwa vizuri kumsikia Sepp Blatter hatimaye akiwa wazi kuhusu haja ya kufanywa mabadiliko lakini tunahitaji kumwona akitumia ushawishi wake kushinikiza mageuzi maalum”.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman