1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter akataa kufichua uchunguzi kuhusu ufisadi

27 Septemba 2014

Huku akikabiliwa na mbinyo wa kumtaka afichue siri inayozunguka madai ya kuwepo ufisadi katika maombi ya mataifa kuandaa Dimba la Kombe la Dunia, Rais wa FIFA Sepp Blatter ameukataa kabisa wito huo

https://p.dw.com/p/1DM5T
Sepp Blatter Sept 2014
Picha: picture alliance/empics

Blatter alionekana kusimama kidete na kukataa kata kutangazwa hadharani kwa ripoti iliyotolewa na wakili kutoka Marekani Michael Garcia baada ya kuchunguza madai ya ufisadi unaodaiwa ulitawala katika mikutano ya kamati kuu ya FIFA iliyotangaza nchi wenyeji wa vinyang'anyiro vya Kombe la Dunia 2018 na 2022

Wakili huyo alipendekeza ripoti hiyo itangawe wazi lakini Blatter anapinga ''maswala ya ndani ya FIFA kuwekwa hadharani''. Rais huyo wa FIFA anasema kuwa shirikisho hilo linasimamiwa na kanuni ambazo haziruhusu uwazi huo.

Kauli ya kuchapisha ama kutochapisha sasa inategemea uamuzi wa mkuu wa kitengo cha kupambana na ufisadi wa FIFA Hans-Joachim Eckert. Dimba la Kombe la Dunia mwaka 2018 litaandaliwa Urusi huku lile la 2022 likiandaliwa Qatar. Rais wa FIFA amepinga kuchapishwa kwa ripoti ya uchunguzi ya wakili Michael Garcia

Mbali na wakili Garcia, makamu wa rais wa FIFA , Jeffrey Webb, mwanamfalme Ali bin Al-Hussein wa Jordan na Jim Boyce pia wametangaza hamu ya kuwekwa wazi sehemu ya ripoti hiyo.

Wakati huo huo, Blatter, ametangaza rasmi nia ya kuwania uchaguzi wa rais wa shirikisho hilo kwa muhula wa tano mfululizo. Tayari mashirikisho ya soka barani Afrika na Asia yametangaza kumuunga mkono Blatter katika kuwania urais.

Blatter, alimthibitisha Issa Hayatou ambaye ni mkuu wa shirikisho la soka la Afrika CAF kuwa naibu mkuu wa rais wa FIFA. Hayatou amechukua nafasi ya Julio Grondona, aliyefariki mwezi Julai

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed KHELEF