Blinken aiomba Uturuki kuiidhinisha Sweden kuingia NATO
31 Mei 2023Blinken aidha amesema Sweden, taifa la Nordic tayari imechukua hatua muhimu za kushughulikia pingamizi zilizokuwa zimetolewa na Uturuki juu ya uanachama wake. Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson mjini Lulea, Blinken amesema Marekani itaendelea na jukumu lake la kukamilisha uwanachama wa Sweden ndani ya NATO kwa wakati kabla ya mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo utakaofanyika katikati ya mwezi Julai na ambao utawaleta pamoja wakuu wa nchi za jumuiya hiyo. Blinken ameongeza kuwa, huu ndio wakati mwafaka wa kuendelea mbele na mchakato huo kwani Sweden na Finland zimeshughulikia wasiwasi uliotolewa na Uturuki. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani pia amekanusha madai kuwa utawala wa Biden ulihusisha hatua ya Uturuki kuidhinisha uanachama wa Sweden kwa NATO na uuzaji wa ndege za kivita aina ya F-16 kwa Ankara. Sweden na Finland zilituma maombi ya kujiunga na NATO mwaka jana baada ya Urusi kuivamia Ukraine.
Soma Zaidi: Erdogan ameashiria ataunga mkono kuikaribisha Finland NATO