1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken akutana na viongozi Kenya

17 Novemba 2021

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amefanya mazungumzo ya faragha na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kuhusu usalama wa kanda, mabadiliko ya tabia nchi na janga la covid 19. Blinken yuko ziarani Afrika

https://p.dw.com/p/436ns
Antony  Blinken
Picha: Andrew Harnik/Pool/AP/picture alliance

Blinken ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya siku tatu, ameelezea wasiwasi wake kuhusu mizozo inayoshuhudiwa katika kanda hiyo, haswa nchini Ethiopia na kuwakata raia wa Marekani walioko nchini humo kuondoka mara moja. 

Mkutano wa Jumatano katika ikulu ya Nairobi unafuatia mazungumzo kati ya Rais Kenyatta na mwenzake wa Marekani Joe Biden yaliyofanyika Wahington DC, nchini Marekani, mwezi Oktoba mwaka huu. Ujio wake Blinken unajiri huku maswali yakiulizwa kuhusu kujitolea kwa serikali ya rais Joe Biden kukabiliana na mizozo inayolikabili bara la Afrika.

Changamoto za kiusalama, zikishuhudiwa nchini Kenya, Ethiopia, Uganda na Somalia. Blinken amelezea Kenya kuwa kiongozi wa kulinda kanda hii na kuimarisha usalama katika upembe wa Afrika. Wakati huo huo, ametoa tahadhari kwa raia wake kuondoka nchini Ethiopia. "Mzozo uliko Ethiopia, ni kitisho cha usalama kanda nzima ya upembe wa Afrika. Mzozo huo unatupa wasiwasi pamoja na washirika wetu. Makundu yanayozozana yaje kwenye meza ya mazungumzo na kuweka kando uhasama wao.” Amesema Blinken

Raychelle Omamo und Antony Blinken
Mzozo wa Ethiopia umekuwa mada kuu ya mazungumzoPicha: Andrew Harnik/Pool/AP/picture alliance

Aidha Kenya na Marekani zimeahidi kufanya kazi pamoja kukabiliana na ugaidi, kutoa ulinzi mipakani, usalama wa baharini na kuhakikisha kuwa vikosi vyao vinadumisha utaalamu katika utendajikazi wao. Mataifa hayo yameapa pia kuendelea kuyashinikiza makundi ya kigaidi katika upembe wa Afrika kupitia ushirikiano wa wanajeshi wao.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Rais Kenyatta ameipongeza Marekani kwa kurejea katika meza ya mazungumzo ya Mwafaka wa Paris akisema kuwa Kenya inatazamia kushirikiana na taifa hilo kusukuma ajenda ya mabadiliko ya tabianchi.  Blinken pia alifanya mazungumzo ya ushirikiano wa kiuchumi na mahusiano na balozi Raychelle Omamo ambaye ni Waziri wa masuala ya kigeni nchini Kenya. "Tumejadili jinsi tunavyoweza kuboresha biashara na uwekezaji, tukagusia pia udumishaji wa amani, inayohitajika katika bara hili, Tumejadili pia masuala ya mazingira.” Amesema Omamo. 

Marekani imeahidi kuendelea kuisaidia Kenya kuboresha asasi yake ya afya na kufikia malengo ya kutoa huduma bora za afya kwa kila mwananchi. Tayari Kenya imepokea zaidi ya chanjo milioni nne za UVIKO, mbali na vifaa vyenye kima cha dola milioni 76 za kukabiliana na janga hilo. Mapema Mwanadiplomasia huyo mwenye cheo cha juu nchini Marekani alikutana na asasi za kiraia, na kuelezea umuhimu wa Kenya juu ya kuandaa uchaguzi huru na wa haki mwakani.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi